November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Mwinyi kuzindua wiki ya sheria Dodoma

Na Zena Mohamed,TimesMajiraOnline,Dodoma

RAIS wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt.Hussein Mwinyi anatarajiwa kuzindua Maadhimisho ya wiki ya Sheria yatakaofanyika Jijini Dodoma Januari 23 mwaka huu.

Kutokana na ujio wa sherehe hizo Mtaka,amezitaka ,Tasisi zote  za Serikali,binafsi,makundi mbalimbali,wadau wote wa mahakama na wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma kwa ujumla na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kwenye sherehe hizo za maadhimisho ya wiki ya Sheria kitaifa.

Hayo yameelezwa jijini hapa leo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka,wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo alisema sherehe hizo za uzinduzi zitaanza kwa zoezi la matembezi yatakayoanzia saa 12:00 asubuhi katika viwanja vya kituo Jumuishi Cha haki(Jengo jipya la mahakama karibu na hazina) na kuishia kwenye viwanja vya Nyerere square ambapo sherehe za uzinduzi huo zitafanyika.

“Wakazi wa mkoa wa Dodoma na jirani mjitokeze kwa wingi katika maadhimisho ya wiki ya Sheria kitaifa Januari hadi Januari 29 mwaka huu na siku ya kilele Februari 1 mwaka huu ,kuungana na viongozi wetu Mhe.Mama Samia Rais wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania,Mhe.Dkt.Hussein Mwinyi Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Muhimili wetu wa Mahakama,”amesema Mkuu wa Mkoa.

Ameeleza kuwa Maadhimisho hayo ya wiki ya Sheria yatafanyika kwa wiki nzima yakijumuisha shughuli uzinduzi wa bendera ya Mahakama,Januari 23,uzinduzi wa Mahakama ya wilaya ya chemba ,Januari 25,uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa Jengo la makao makuu ya mahakama ya Tanzania-judicial square Januari 26 na Uzinduzi wa Mahakama ya wilaya ya bahi January 28 mwaka huu.

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Bernard Mpepo amesema kwenye maadhimisho hayo pia kutakuwa na uzinduzi wa majarida na sheria mbalimbali zinazohusu Mahakama zitakazofanywa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.

Sherehe za maadhimisho ya wiki ya Sheria kitaifa zitafanyika kwenye Mkoa wa Dodoma Makao Makuu ya Nchi kuanzia Januari 23 hadi Januari 29 mwaka huku kilele chake  kikifanyika Februari 1 mwaka huu ambapo mgeni rasmi atarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.