Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii ,Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima Dkt. Gwajima amesema,mpango wa Serikali ni kuwaondoa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi (mitaani) na kuwarejesha kwenye mazingira bora kupitia makao ya watoto nchini kote ambapo kwa sasa kuna jumla ya vituo 468 .
Aidha Waziri huyo amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.Zainab Chaula kushirikiana na wamiliki wa vituo binafsi na kufanya tathmini ya uwezo na utayari wa vituo vyote namna vinavyoweza kuwa sehemu ya utekelezaji wa zoezi hilo.
Dkt.Gwajima ameyasema hayo alipotembelea Makao ya Taifa ya kulelea watoto Kikombo, mkoani Dodoma.
Amesema, taarifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inakadiriwa kuwa, jumla ya watoto milioni 2.5 walikuwa wanaishi na kufanya kazi mitaani kufikia mwaka huo sawa na asilimia 12 ya watoto wote nchini.
Vile vile Dkt.Gwajima amezitaka Taasisi za Ustawi na Maendeleo ya Jamii nchini kuimarisha ushirikiano na jamii zinazowazunguka ili kuhamasisha, kuelimisha na kubuni mbinu zitakazoiwezesha jamii kujiendeleza na kuepusha watoto na vijana kukimbilia mijini na kujiingiza kwenye ajira zisizo rasmi na kuharibu ndoto za maisha yao.
“Siku ya jumatatu(Januari 17,2022) tulikutana na watoto waishio kwenye mazingira hatarishi (mitaani) hapa Dodoma na katika kuwasilikiza wapo baadhi yao unawaona kabisa wanao mwelekeo lakini wamekosa wa kuwaongoza njia sahihi na hivyo kuamua kutoroka majumbani na kukimbilia mijini” amesema Dkt. Gwajima na kuongeza kuwa
“Lakini kama vyuo vyetu vikiliona hili na kuisaidia jamii tunaweza kupunguza wimbi la watoto kukimbilia mijini.
Naye Naibu Waziri wa Wziara hiyo Mwanaidi Ali Khamis amewaasa Maafisa Ustawi wa Jamii katika Makao hayo, kuhakikisha wanawalea Watoto kwa kuzingatia maadili, taratibu na miongozo mbalimbali iliyopo kuhusu Malezi na Makuzi ya Mtoto.
“Jukumu letu hapa nikutoa Malezi ambayo mtoto angeweza kuyapata akiwa kwa mzazi wake, hivyo sisi kama jamii tulioamua kubeba dhamana hii lazima tuoneshe mapenzi mema kwa watoto hawa ili waweze kujiona wana thaminiwa na jamii yao” amesema Mwanaidi
Akizungumza wakati wa kikao hicho Katibu Mkuu Dkt. Zainabu Chaula, alisema amepokea maelekezo hayo kwa utekelezaji huku akiahidi kusimamia na kuhakikisha kuwa, Makao ya Taifa ya Watoto na mengine nchini kote yanajielekeza kwenye kutoa Watoto watakaoweza kujitegemea na kufika mbali kwa kupatiwa stadi mbalimbali ili waweze kuchangia katika uchumi na maendeleo ya Taifa.
Awali akitoa taarifa ya kituo hicho, Afisa Mfawidhi wa Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo Vivian Kaiza, amesema maono ya kituo hicho ni kuwa cha mfano kitaifa katika kuwalea Watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na kufanya kazi zisizo rasmi kwa kuwapatia Malezi na Makuzi ya stadi za kazi kwa lengo la kujitegemea baadaye.
xxxxxxxx
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa