November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa: Wagonjwa Corona wazidi kupungua nchini

Na Joyce Kasiki, Dodoma

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema idadi ya wagonjwa wa corona imeendelea kupungua huku baadhi ya vituo vikiwa havina wagonjwa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwahutubia Waumini wa Dini ya Kiislam, baada ya sala ya Eid el Fitri, katika Msikiti wa Gaddafi, Jijini Dodoma, May 24, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Akizungumza mara baada ya sala ya Idd El Fitri katika msikiti wa Gaddafi jijini Dodoma, Waziri Mkuu amesema, licha ya wagonjwa kupungua bado hatua za kujikinga zinapaswa kuchukuliwa ili ugonjwa uendelee kupungu.

“Kwa mujibu wa takwimu za leo asubuhi Dar es Salaam kuna wagonjwa 11, Kibaha 16 na Dodoma kituo cha Mkonze wagonjwa ni watatu” amesema Majaliwa

Amesema, takwimu kuonyesha maambukizi kushuka ni nzuri lakini jambo kubwa kwa sasa ni kuendelea kuchukua tahadhari ili kuzuia uwezekano wa mtu kuambukiza na kuambukizwa huku akiwataka wananchi kuendelee kuchukua tahadhari zote zinazotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wataalam wa Afya.

“Naomba tuendelee kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni na njia zote zinazozuia maambukizi kutoka mtu mmoja hadi mwingine” amesema Waziri Majaliwa.

Waumini wa Dini ya Kiislamu, waliyohudhuria katika ibada ya sala ya Eid el Fitri, akiitikia dua, baada ya sala, katika Msikiti wa Gaddafi, Jijini Dodoma, May 24, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Hata hivyo amewataka wananchi kuutumia uhuru wa kufanya shughuli zao zote bila kuvuka mipaka na kumtaka kila Mtanzania kwa dini yake kumwomba Mwenyezi Mungu atuepushe na janga la corona kama alivyoagiza Rais Dkt. John Magufuli.

Akizungumza kuhusu amani, Majaliwa amesema, wananchi waendelee kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu ili kuidumisha amani iliyopo nchini na kuendelea kuifanya Tanzania kuwa ni kisiwa cha amani na mataifa mengi kuifanya kuwa kimbilio.

“Tanzania imekuwa mfano kwa nchi nyingine zinazotamani tunu hiyo na kuifanya nchi yetu kuwa kimbilio, tuendelee kuienzi ili iendelee kudumu” amesisitiza Waziri Majaliwa.

Awali, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rajab Mustapha amewaasa waumini wa madhehebu mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuacha kufanya machukizo mbele za Mwenyezi Mungu ili atuepushe na majanga mbalimbali likiwemo la Corona.

“Tumeomba dua kwa Mwenyezi Mungu tumeitikiwa, tusirejee kumuasi, watu wasifanye mabalaa, wasishabikie kwa kufungua baa, ulevi, kwani Mungu atarudisha janga kuliko lilivyokuwa awali” amesema Sheikh Mustapha na kuongeza

“Tuwe wenye kushukuru na siyo kukufuru rehema na Mungu, tuendelee kumwomba ili atokomeza kabisa janga hili la Corona na kumuelekea Mungu kwani Corona haitachukua muda wala haitapata nafasi nchini lakini kubwa ni kuendelea kuchukua tahadharai za wataalamu wa afya,” amesema Sheikh Mustapha.