Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kimewataka walimu wote wa chama hicho Mkoa wa Morogoro kupuuza taarifa zote ambazo zimejitokeza hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii ambazo zinaleta taharuki na kupelekea kukosa amani ya kufanya kazi zilizotolewa na kikundi ambacho kimejitokeza na kuongea mambo yasiyofaa.
Baadhi ya mambo ambayo waliyoyaongea wanakikundi hao ni kuhusu T-shirt ambazo wanadai hazijawafikia wanachama wa Mkoa wa Morogoro ambapo wanachama wote wa chama hicho Cha walimu Mkoa wa Morogoro wamepata T-shirt hizo.
Akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), Jumanne Nyakirang’ani amesema inawezekana Kundi hilo limetumwa na watu waliosimamishwa uongozi hivyo amewataka walimu wa wanachama wote wa chama hicho kupuuza taarifa hizo na kuendelea kutoa kushiriako kwa serikali ili iendelee kuwahudumia;
“Tunachohitaji utulivu uliopo ndani ya Chama chetu Cha walimu na walimu kwa ujumla tunaomba uendelee na waupatie serikali ushirikiano mkubwa ili serikali iendelee kutuhudumia kwa kushirikiana na chama chetu Cha walimu”
Mbali na hayo Mwenyekiti huyo amesema serikali inaendelea kuwahudumia walimu kwa kuwapandisha madaraja na watumishi wengine;
“Serikali inaendelea kuwahudumia walimu mfano, suala la madaraja, mwaka 2021 walimu wamepandishwa madaraja na watumishi wengine zaidi ya laki moja lakini kwa wingi wetu sisi walimu ndiyo tunaongoza”
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa wanaendelea na mazungumzo na serikali ili walimu waendelee kupanda madaraja na utaratibu unaendelea kutolewa na chama Cha Walimu makao makuu kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu
Nyakirang’ani amesema Chama Cha walimu kimetoa mafunzo mwaka 2021 kwa viongozi wote wa chama Cha walimu kuanzia ngazi ya shule hadi ngazi ya Taifa na sasa mwaka 2022 wanakwenda kutoa mafunzo kwa wanachama wao wote baada ya kuwa viongozi wa chama Cha walimu kupata mafunzo.
Pia Nyakirang’ani ameipongeza serikali ya awamu ya Sita iliyopo chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa wanayoifanya na wanayoendelea kuifanya katika kuhakikisha elimu inapewa kipaumbele;
“Tunaipongeza serikali yetu chini ya uongozi wa Rais mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kutuletea maendeleo hasa katika suala la elimu mfano amejenga madarasa nchi nzima ambapo walimu wetu watafanya kazi wakiwa katika mazingira mazuri ya kuwafundisha wanafunzi wetu ingawa bado anaendelea na jitihada za kuendelea kuwasaidia walimu kwa kusaidiana na chama Cha walimu hasa kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu”
Mwenyekiti huyo alimaliza kwa kuipongeza Ofisi ya Katibu Mkuu chama Cha walimu kwa kazi kubwa inayoifanya kushirikiana na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
More Stories
Wananchi Babati wamshukuru Rais Samia kwa kuwafungulia barabara
Rais Samia aungwe mkono ajenda ya nishati safi ya kupikia
Ushiriki wa Samia G20 wainufaisha Tanzania