November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mchengerwa aelekeza walengwa wa TASAF kupewa ruzuku kabla ya krismasi na Mwaka mpya

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Waratibu wa TASAF nchini kuhakikisha walengwa wanapewa ruzuku kabla ya Sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya ili waweze kujipanga mapema kuboresha maisha yao. 

Akizungumza na wananchi na walengwa wa TASAF katika Kijiji cha Kazuramimba, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Waziri Mchengerwa amesema Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alishatoa maelekezo ya kuwapatia ruzuku walengwa wa TASAF mara baada ya kukamilika kwa zoezi la uandikishaji na uhakiki. 

“Waratibu wa TASAF hakikisheni walengwa wa Kazuramimba wanalipwa kwa wakati kabla ya Krismasi ili wapange mikakati madhubuti itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi katika Mwaka Mpya unaokuja,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Akizungumzia azma ya Serikali ya kuwahudumia wananchi, Mhe. Mchengerwa amesema, Serikali isiyowajali walengwa wa TASAF ni sawa na Serikali isiyokuwa na huruma kwa wananchi wake na kukosa hofu ya Mwenyezi Mungu.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, dhamira ya Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuzifikia kaya milioni moja na laki tano ambazo ni sawa na Watanzania milioni kumi na tano ambao watanufaika na mpango wa kuzinusuru kaya zenye uhitaji.

Waziri Mchengerwa amesema, Baba wa Taifa alisema kama Taifa hatutaweza kupiga hatua iwapo Watanzania wengi wana hali duni ya maisha na ndio maana Serikali ya Awamu ya Sita imeamua kuzikwamua kaya zisizojiweza kupitia mpango wa TASAF.

Katika kuhakikisha miradi ya TASAF inatekelezwa ipasavyo, Mhe. Mchengerwa amesema akiwa ndiye Waziri mwenye dhamana ya kumsaidia Mhe. Rais kusimamia utekelezaji wa miradi ya TASAF, atahakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili kutimiza azma ya Mhe. Rais kuzifikia kaya zote zenye hali duni nchini.

Mhe. Mchengerwa amehitimisha ziara ya kikazi mkoani Kigoma yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.