November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri wa Ujenzi achukizwa na kasi ya ujenzi wa barabara

Na Hadija Bagasha Tanga,

Naibu Waziri wa Ujenzi na uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya ameonyeshwa kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara ya Pangani – Tanga inayojengwa na mkandarasi kutoka kampuni ya China (CHIKO) ambayo kwa sasa ipo kwa asilimia 20 muda ambao ilitakiwa iwe imekamilika huku akibainisha kuwa zipo barabara nyingine nchini ambazo zimejengwa na mkandarasi huyo anayejenga barabara hiyo ambazo zimefeli na kuwataka wanaomsimamia kuwa makini naye.

Pia amemuagiza Mhandisi Mshauri kuhakikisha mkandarasi huyo anafanya kazi kama kazi ilivyoainishwa kwenye mkataba na kufuata michoro yote na dizaini kama zilivyo huku akibainisha kuwa zipo barabara nyingine nchini ambazo zimejengwa na mkandarasi huyo ambazo zimefeli.

Awali akizungumza mara baada ya kukagua barabara hiyo ya Tanga-Pangani Naibu waziri huyo amesema kuwa ameshawahi kukagua moja ya barabara ambayo imetengenezwa na mkandarasi huyo ambayo nusu ya barabara iliyojengwa inafumuliwa kuanzia chini lakini mkandarasi huyo alifanya kazi chini ya wahandisi washauri wakiwepo pamoja na Tanroads.

“Kwa kampuni kubwa kama kufumua barabara kama kilomita 7 kuanzia mwanzo na washauri walikuwepo ni jambo la kushangaza sasa hili naomba lisije kutokea kwenye barabara hii na kila hatua Tanrods mjiridhishe kwamba kila hatua tunayokwenda hawa watu wametekeleza kwa kiwango naongea sababu hawa watu wamefanya moja ya barabara ya Mwigumbi-Maswa sio siri hiyo barabara inafumuliwa katika sehemu kubwa ya barabara kwa hawa hawa Chiko, “alibainisha naibu waziri.

Naibu waziri huyo amemuagiza mkandarasi mjenzi wa barabara hiyo kuhakikisha inajengwa kwa kiwango cha juu kwa kuzingatia ubora na viwango kutokana na gharama kubwa serikali iliyotumia katika barabara hiyo.

Aidha alisema kwa mkandarasi anatakiwa aelezwe kwamba pengine wanahitaji kuwa na jicho la ziada sababu wameona baadhi ya barabara walizojenga zikifeli na kutolea mfano barabara ya Mwigumbi-Maswa ambayo hivi sasa imefumuliwa na kuanza kujengwa upya.

Naibu waziri huyo alisema kwao kama serikali jambo hilo linawarudisha nyuma na hiyo ni kutokana na watu hawakuwajibika katika nafasi zao hivyo ameeleza kuwa hawataki jambo hilo litokee Mkoani Tanga hivyi ipo haja ya kuliangalia sana kwani serikali haitakubali barabara kama hiyo ifeli mapema.

“Mwambieni mkandarasi Chiko ni kampuni kubwa na tunaamini ina uwezo mkubwa hatuwezi kusema inasimama kwa sababu imecheleweshewa fedha za serikali bilioni moja au mbili sidhani kama ni sahihi tunachotaka hawa watu wafanye kazi usiku na mchana muhimu kujali muda, ubora wa barabara, tunahitaji kuwasimamia sana hawa watu, “alisistiza Naibu waziri Kasekenya.

“Mhandisi mshauri mimi nimetembelea barabara nyingi sana lakini kuna barabara ambazo zimefeli mapema sana haijalishi kama mkandarasi atarudia kwa gharama zake lakini hata kama atarudia kwa gharama zake kama Taifa au watumiaji anakuwa ameturudisha nyuma sanaa sababu muda tuliotaka kuitumia haijakamilika.,”alisistiza naibu waziri huyo.

Hata hivyo Naibu waziri huyo alisema pesa inayotolewa ni ya Watanzania hivyo hatovumilia kuona barabara zinatengenezwa chini ya kiwango wakati huo kampuni inayosimamia ni kampuni ya Kitanzania ambayo ni fahari kubwa kupewa kazi kama hiyo.

Amesisitiza kuwa hatakubali serikali itoe gharama kubwa halafu ipotee na kwamba serikali haipo tayari kuona kwenye kazi zake na uwekezaji mkubwa kama huo kazi zinafanywa chini ya kiwango na ukizingatia kampuni hizo ni za kimataifa.

“Mkandarasi huyu akifanya vibaya hizi ni kampuni za kimataifa ambazo zinafanya kazi dunia nzima na sisi tukisema hawafai hawatapata kazi sehemu nyingine hii ni kwa wakandarasi wote, “

Kwa upande wake meneja wa Tanroads Mkoa Tanga Mhandisi Alfred Ndumbaro alisema mkandarasi Chiko alianza kazi hiyo mwezi Novemba 15 mwaka 2019 wakati anakabidhiwa kulikuwa na changamoto ya ugonjwa wa corona na hivyo kushindwa kuleta wataalamu kutoka Nchini Chini kwa wakati mpaka mwezi mwezi May 2020 ndio alipoanza rasmi.

“Mheshimiwa waziri kazi inaendelea kwa taratibu kwa sasa kafikia asilimia 20 lakini kazi hii alitakiwa akabidhi serikalini barabara hiyo tarehe 15 mwezi Novemba 2021 laini haikuwezekana kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ugonjwa wa corona na serikali kuchelewa kumlipa fedha za kianzio, “alisema Mhandisi Ndumbaro.

Mhandisi Ndumbaro anasema tayari serikali imeshatoa zaidi ya bilioni 4 kwajili ya kulipa fidia kwa wananchi na kueleza kuwa hivi sasa maeneo yaliyobaki na migogoro ni machache ambayo wanaendelea nayo .

Naye Mhandisi Yohakim Mbwale ambaye ni mhandisi msimamizi amesema wanatarajia kukabidhi barabara hiyo mwezi April 2023 lakini pia wamepokea maelekezo ya waziri juu ya kuzingatia muda na viwango licha ya changamoto mbalimbali ambazo wamekuwa wakikutana nazo.

“Mkandarasi ameomba tuongezewe wa siku 525 lakini uchambuzi umeonyesha aongezwe siku 523 kwahiyo matarajio ni kwamba barabara itaisha mwezi April 2023,”alisema mhandisi huyo.

Ujenzi wa barabara ya Tanga-Pangani ina urefu wa kilometa 50 yenye thamani ya shilingi bilioni 66.8 na kujengwa na mkandarasi Kampuni ya China Henan International Company Limited(CHICO).