Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Serikali imepiga marufuku kuweka matangazo ya ushauri kwenye maduka ya uuzaji wa dawa za binadamu kwani ni kinyume na kifungu namba 46 (c) kinacho simamia usajili wa maduka.
Akiongea na waandishi wa Habari leo jijini Dodoma, Msajili wa Baraza la Famasi Elizabeth Shekalaghe amesema maduka ya dawa sio hospitali hivyo kuweka matangazo ya kutoa ushauri wa kitabibu ni kukiuka taratibu za vibali vya usajili wa maduka hayo.
“Nitoe wito kwa watu wote wenye maduka ya dawa, ni marufuku kuweka matangazo ya kujinadi kwamba unatoa ushauri na picha ya Daktari umeiweka hapo ukutani, nirudia kusema kawaambieni hili halikubaliki na yeyote atakaye kwenda kinyume na utaratibu uliowekwa kwenye maduka ya dawa Sheria itachukua mkondo wake”. Amesema Shekalaghe.
Shekalaghe, ameonya pia wale wote wanaoendesha maduka ya dawa bila kujisajili (Maduka bubu), ambapo amesema katika siku za hivi karibuni kumeibuka tabia kwa ya baadhi ya wenye maduka ya dawa wasio waaminifu kwenda kinyume na seria na kujianzishia maduka bila kufuata utaratibu wa usajili, kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Amewaomba wananchi kutoa ushirikiano pindi waonapobaini biashara duka la dawa inaendeshwa kwa kuuza dawa bila ya kuwa na usajili wala na Nembo ya Msajili ambayo kimsingi inapaswa kubandikwa kwenye duka husika.
Shekalaghe amewakumbusha wananchi faida za matumizi sahihi ya dawa ambayo yanaweza kupunguza uwezekano wa kujenga usugu kwa vimelea vya magonjwa, kupunguza madhara/ maudhi ya dawa na hupunguza gharama za matibabu kwa mgonjwa na Serikali.
Baraza la Famasi ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, iliyoundwa na Sheria Na.1 ya Famasi Sura 311 ikiwa na jukumu kubwa la kusimamia taaluma ya famasi nchini, hususani usajili wa wanataaluma wa fani ya famasi na kusimamia utendaji wao, usajili wa majengo yanayotoa huduma za dawa pamoja na utambuzi wa vyuo vinavyofundisha fani ya famasi.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi