Na Mwandishi wetu,timesmajira,Online
WAGANGA wa Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini, wametakiwa kujisajili,kuorodhesha wasaidizi wao,kusajili vituo,pamoja na Dawa wanazotumia kutibu wagonjwa kabla ya Machi 31,2022.
Agizo hilo limetolewa leo mkoani Dodoma na Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Mbadala,Prof.Hamis Malebo wakati akiongea na waandishi wa habari,amesema kuendelea kufanya matibabu bila kupata kibali kutoka katika Baraza la Tiba Asili na Mbadala ni kosa kisheria.
Amesema wale wote wanaoendelea kutoa huduma bila kusajiliwa wanatakiwa wawe wamejisajili kabla kufikia machi 31, 2022, baada ya hapo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“Nawataka waganga wote kujiepusha na vitendo vyote vinavyokinzana na Sheria, kanuni na taratibu zilizopo, ikiwa ni pamoja na kuacha kuweka mabango yanayopotosha jamii, kurusha matangazo kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii bila ya kuwa na Kibali kutoka Baraza la Tiba asili nchini,” amesema Prof. Malebo
Aidha aliwataka wauza dawa kiholela kwenye vyombo vya usafiri, nyumba za ibada, sokoni na sehemu zenye mikusanyiko kuacha tabia hiyo kwa kuwa dawa zote za asili zitauzwa katika maduka ya dawa yaliyosajiliwa.
Hata hivyo Prof. Malebo amewataka wanaotoa elimu za Tiba Asili na Mbadala kwenye Vituo vya Redio na Runinga nao kupata kibali kutoka Baraza.
Kwa upande wake Msajili-Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala Dkt. Ruth Suza amewataka waganga kuwamakini katika utoaji wa huduma sababu wanahusika moja kwa moja na Afya za wananchi.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi