November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Marufuku kubeba watoto chini ya miaka 8 mshikaki

Na Martha Fatael, TimesMajira Online, Moshi

JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro, limepiga marufuku waendesha pikipiki za abiria maarufu kama Bodaboda kubeba watoto zaidi ya mmoja katika pikipiki kwani ni hatari kwa maisha ya watoto hao.

Aidha wazazi na walezi wameombwa kukagua magari yaliyotengwa kwa ajili ya kubeba wanafunzi kwani baadhi ya magari hayo yamebainika kuwa ni chakavu na hatarishi kwa watumiaji.

Mkuu wa kikosi Cha usalama barabarani mkoani Kilimanjaro, Zauda Mohamed amesema hayo akihimiza wenye vyombo vya moto kufanya ukaguzi wa vyombo vya usafiri kama sehemu wiki ya usalama barabarani iliyofanyika kitaifa jijini Arusha.

Akizungumzia katika mahojiano maalum na mpango wa malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto (ECD) unaotekelezwa na Muungano wa vilabu vya wanahabari nchini UTPC kwa ufadhili wa Ireland, Zauda amesema watoto wanahitaji uangalizi wa zaidi.

Amesema baadhi ya watoto katika Shule za awali, ambao hupelekwa Shule alfajiri Sana, husinzia pale wanapopakia pikipiki hivyo ni hatari na wanaweza kuanguka na kujeruhiwa ama kupoteza maisha.

“Ni jukumu la wamiliki wa Shule kuhakikisha magari yanafanyiwa matengenezo lakini ni wajibu wa wazazi na walezi kujiridhisha kuhusu usalama wa watoto wao waendapo na kurudi Shule” amesema.

Hata hivyo Mwenyekiti wa chama Cha waendesha bodaboda mkoani Kilimanjaro, Bahati Nyakiraria amesema sheria ya usalama barabarani inakataza watoto Chini ya miaka nane kupanda pikipiki isipokuwa Bajaji kwa uangalizi maalum.

Aidha Nyakiraria amesema tayari uongozi ulitoa maelekezo kwa waendesha pikipiki na Bajaj kuhusu angalizo maalumu kwa wanafunzi chini ya miaka nane kutopanda Bajaj na pikipiki wakiwa wenyewe bali ni lazima kuwa na mtu mzima ambaye atakuwa mwangalizi wao.

Amesema yapo baadhi ya matukio ya ajali zinazohusisha watoto Chini ya miaka nane lakini siyo zote zinaripotiwa katika jeshi la polisi huku kukiwa na changamoto ya wanaosababisha ajali kutoroka baada ya ajali.

Amewataka wazazi na walezi kuongeza umakini kwa watu wanaowatumia kama madereva wa watoto wao, ikiwemo kuchukua watu wanaowafahamu vyema tabia.

Akizungumza hivi karibuni, kamanda wa polisi mkoani hapa, Simon Maigwa amesema ukaguzi huo ni takwa la kisheria hivyo ni wajibu wamiliki kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi.

“Ukaguzi ni kwa mujibu wa kifungu namba 39, 81, 82 na 83 vya sheria ya usalama barabarani namba 30/1973 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002” amesema.

Kwa upande wake ofisa mkaguzi wa magari ambaye pia ni Ofisa operesheni usalama barabarani mkoa huo, Elias Mkuburo amesema kipindi cha ukaguzi wa hiari ni miezi mitatu kuanzia sasa.

Amesema kwa Sasa hakuna atakayetozwa faini bali wamiliki watashauriwa kufanya matengenezo ya vyombo vyao na watakaokaidi watachukiliwa hatua za kisheria.