November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt Gwajima akutana na watumishi Hospitali ya rufaa Tabora na kutoa maagizo mazito

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima leo Novemba 26, 2021 amewasili Mkoani Tabora na kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya miradi ya Afya inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Afya.

Katika ziara hiyo Dkt. Gwajima ameuagiza uongozi wa Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete kuhakikisha wanamaliza miradi hiyo ili wananchi waanze kupata huduma zilizokusudiwa zikiwemo huduma za matibabu ya dharura, mahututi, afya ya uzazi, mtambo wa kufua hewa ya oxygen na uchunguzi kwa CT scan.

Aidha Dkt.Gwajima amekutana na Watumishi wa afya katika Mkoa huo na kuwaagiza kwenda kujifunza kwa majirani zao wa Mkoa wa Mwanza jinsi gani wamefanikiwa kuongeza Kasi zaidi katika kuchanja wananchi ukilinganisha na Mikoa mingine mingi. Dkt Gwajima ameitaja mikoa ya Mwanza, Kagera na Ruvuma kama yenye Kasi kubwa zaidi katika kuwafikia wananchi kwa chanjo katika Awamu hii ya chanjo ya Sinopharm.

Dkt. Gwajima amesisitiza umuhimu wa kuelimisha wananchi wa mkoa wa Tabora na Tanzania yote kwa ujumla na kuwapatia huduma ya chanjo ya UVIKO 19 kwa kasi zaidi hasa ukizingatia uwepo wa taarifa za kuongezeka kwa maambukizi ya wimbi la nne katika nchi mbalimbali duniani na wanaoathirika zaidi ni wale ambao hawajachanja.

Dkt. Gwajima ametembelea mradi wa jengo la huduma za dharura (EMD) pamoja sehemu ya kufunga mtambo wa kufua hewa Tiba ya oxygen ambayo iko mbioni kukamilika mwishoni mwa Disemba 2021.