November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mchengerwa ataka viongozi TAKUKURU kupimwa kwa usimamizi wa miradi

Na Zena Mohamed,TimesMajira,Dodoma.

VIONGOZI wa Taasisi ya  Kuzuia na Kupambana na  Rushwa(TAKUKURU),wametakiwa kuongeza jitihada katika kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kutambua haki zao ili waweze kuepukana na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa.

Hayo yamesemwa jijini hapa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora Mohamedy Mchengerwa,wakati akifungua  Mkutano Mkuu wa mwaka wa viongozi 60 wa TAKUKURU ,kutoka katika Mikoa 28 , wenye lengo la kujadili utendaji kazi, pamoja na changamoto katika kazi zao.

Vilevile ,Mchengerwa amewaagiza viongozi hao kufatilia vyema  utekelezaji wa miradi yote ya kimaendeleo inayoendelea hapa nchini na wahakikishe kuwa kusiwepo na mianya ya rushwa.

“Utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo umegubikwa na  udanganyifu ninyi kama TAKUKURU kiongozi wa kila wilaya apimwe namna anavyoweza kusimamia  matumizi ya fedha katika kila Wilaya na niseme tu kwamba hili ni  jukumu letu  sote katika kusimamia,

“Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan alivyofungua hizi fursa za uchumi  hakumaanisha watu watumie fedha hizo vibaya  na kutumia nyaraka za uongo kuhusu gharama zinazotumika  katika miradi  hiyo tumieni mkutano huu kujadili malengo na muhakikishe kusiwepo na mianya ya uchepushaji wa fedha hizo kwaajili ya matumizi binafsi katika kila mradi”amesema Mchengerwa.

Aidha amesema Taasisi hiyo inatakiwa isionekane na kasoro ya rushwa  na badala yake iwe mstari wa mbele kufanya kazi usiku na mchana ili kuokoa rasilimali za Taifa .

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Hamis Mkanachi akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthon Mtaka, amewataka  viongozi hao kutumia mkutano huo kujadili tathmini ya mwaka mzima  na zaidi wajikite katika kutatua uzembe  pamoja na kutowajibika kwa baadhi ya viongozi wa Taasisi hiyo.

“Wito wangu kwenu  ni kwamba tathmini yetu iwe ya kina na  tutazame namna tutakavyoweza kujipambanua katika kila Wilaya namna bora ya utendaji” amesema.

Kwa upande wake  Mkurugenzi Mkuu kutoka katika Taasisi ya kuzuia  na kupambana na rushwa  TAKUKURU, Salumu Hamduni,amesema wametekeleza majukumu na kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2021 jumla  ya shilingi billion 29.3 ziliokolewa ambapo billion 11 .2 ziliokolewa kwa mfumo wa fedha taslim  na utaifishaji mali na kiasi cha  bilioni 18 zilidhibitiwa kabla hazijatumika.

Ameeleza miradi ya kimaendeleo 1,188 yenye thamani ya billion 714.17 katika sekta ya  afya maji elimu  ziliweza kufatiliwa na kuona makosa  ambayo wameyachukulia hatua.

“Tumeelimisha katika ngazi ya Makao Makuu pamoja na wakuu wa TAKUKURU, kuzuia vitendo vya rushwa kuelimisha, kushirikisha jamii pamoja na kuwafikisha watuhumiwa Mahakami kwa kushirikiana na ofisi ya Taifa ya  mashtaka ambapo majalada 1,053 yalichunguzwa na kukamilishwa na majadala  339 yaliwasilishwa kwa Mkurugenzi  wa mashitaka kuomba kibali cha kuwafikisha mahakani ambapo kesi mpya  zilipatikana 542, na kesi 541 zilitolewa uamuzi ambapo Jamhuri iliweza kushinda kesi 345”amesema Hamduni

Pia amezungumzia changamoto zinazoikabili Taasisi hiyo amesema ni pamoja na ufinyu wa bajeti ambao umeathiri uchunguzi, mafunzo kwa wafanyakazi, ununuzi wa vifaa na mahitaji mbalimbali  pamoja na uhaba wa wafanyakazi.

Hata hivyo Mkutano huo ambao utadumu kwa siku tatu umebebwa na kauli mbiu isemayo  ” kupambana na rushwa ni jukumu lako”