Na Reuben Kagaruki,TimesMajira,Online,Dar
SERIKALI imeshauriwa kuacha kutumia kigezo cha wingi wa vyombo vya habari vilivyosajiliwa yakiwemo magazeti 270 kama kipimo cha uhuru wa vyombo vya habari nchini, wakati kiuhalisia siyo hivyo.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na mwandishi wa habari mkongwe nchini kutoka Kampuni ya Mwanahalisi, Saed Kubenea wakati akizumgumza kwenye mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao kuhusu Maadhimisho Siku ya Kimataifa ya Utoaji Habari kwa Wote yaliyofanyika juzi.
Maadhimisho hayo yalienda sambamba na mafunzo ya waandishi wa habari za mahakamani ambayo yaliyoandaliwa na Shirika la Internews. Kubenea alipingana na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari (MAELEZO) Kitengo cha Usajili wa Vyombo vya Habari, Patrick Kipangula, ambaye wakati akifungua mkutano na mafunzo hayo alitumia takwimu za vyombo vya habari vilivyosajiliwa nchini yakiwemo magazeti, vituo vya redio, redio za mtandaoni, vituo vya televisheni, televisheni za mtandaoni kuthibitisha jinsi Tanzania ilivyotoa uhuru mpana kwa wanahabari na vyombo vya habari kufanyakazi kwa ujumla.
Kubenea amesema wao ni wahanga wa kufungiwa magazeti na yeye akiwa mmiliki na mwandishi wa habari, amesikitishwa na kauli ya Kipangula, kutumia wingi wa mazeti yaliyosajiliwa nchini kama kigezo cha uhuru wa vyombo vya habari.
Ametoa mifano mbalimbali kuthibitisha hoja yake, ikiwemo wa magazeti ya Kiswahili yanayotoka kila siku kubaki matano mitaani. Alifafanua kwamba magazeti mengine hayatoki kabisa na mengine yanasomwa mitandaoni, lakini mitaani hayapo.
Aidha, ametolea mfano wa gazeti lake la Mwanahalisi, akisema lilipewa adhabu ya miezi 24 kutochapishwa kuanzia Septemba 10, 2017 na waliambiwa baada ya adhabu hiyo wanaweza kuomba leseni upya, kwa maana watakuwa wamejirekebisha.
Kwa mujibu wa Kubenea walikata rufaa mahakamani na walishinda na baadaye Serikali ilikata rufani, lakini ilishindwa, lakini hadi leo ni miezi 48 gazeti hilo halijapata usajili.
Aidha, alitolea mfano wa gazeti lake la Mseto, ambalo nalo lilifungiwa na Serikali. Mifano mingine aliyoitoa ni ya magazeti ya Tanzania Daima, Raia Mwema na mengine. “Kwa hiyo kusema Tanzania kuna uhuru na haki kwa vyombo vya habari hayo ni maneno yaliyoandikwa kwenye vitabu (sheria), lakini utekelezaji haupo,” amesema Kubenea.
Aliituhumu Idara ya Habari Maelezo kuwa imekuwa mlalamikaji, mwendesha mashtaka na mtoaji hukumu kwa vyombo vya habari, jambo ambalo alidai halitoi uhuru kwa vyombo hivyo.
Akijibu hoja ya Kubenea kuhusu kufungiwa kwa baadhi ya magazeti Kipangula alisema Serikali inao wajibu wa kulinda maadili ya vyombo vya habari ili kuhakikisha habari zinazotolewa zina taarifa sahihi.
Alifafanua kwamba vyombo vile vinavyofungiwa vina haki kuonba leseni upya na kwamba hata mchakato wa kutoa leseni kwa magazeti ya kampuni yake (Kubenea) unaendelea.
Awali akifungua mafunzo hayo, Kipangula amesema Serikali ina wajibu wa kuhakikisha vyombo vya habari na wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati na kwamba hilo ni takwa la sheria.
“Utoaji wa taarifa za Serikali ni takwa la Kisheria, hivyo ni lazima taarifa zote zitolewe isipokuwa zile ambazo zinakatazwa na sheria. Akisisitiza hilo, amesema Kifungu cha 7 (1) cha Sheria ya Huduma za Habari kinaruhusu uhuru wa kutafuta, kuchakata na kutangaza habari.
Hata hivyo, amesema hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa kwa vyombo vya habari ni kwa lengo la kudhibiti upotoshaji wa taarifa ili kulinda maadili ya taaluma ya habari.
Kwa msingi huo, amesema mafunzo hayo kwa waandishi wa habari za mahakamani yatawasaidia kubadilika na kutoa taarifa kwa usahihi. Kwa upande wake ofisa habari wa mahakama, Faustine Kapama, aliwataka wanahabari wanaporipoti habari za mahakama kuhakikisha pande zote zinatendewa haki, pamoja na habari hizo kuandikwa kwa usahihi.
Amesema pamoja na wanahabari kuruhusiwa kuripoti habari za mahakama, lakini ni muhimu kujua mipaka ya kazi zao.
Naye Ofisa Programu, Uwazi na Upatikanaji Habari wa Shirika la Article 19 la nchini Kenya, Sarah Mwesonga ameshauri Serikali za Afrika Mashariki na Kati kupitia upya sheria zake za habari na kuziwekea viwango vya kimataifa vya uhuru wa upatikanaji wa habari ikiwa ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa sheria hizo, kwani kila mtu ana haki ya kutafuta na kupata habari.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti