November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakandarasi wasisitiza kuheshimu mikataba

Na Veronica Simba,TimesMajira Online,Tabora

SERIKALI imewataka Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini nchini kote kuheshimu makubaliano ya utendaji kazi yaliyoafikiwa baina ya pande hizo mbili kupitia mikataba waliyosaini.

Ujumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini ukikagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini katika Kijiji cha Igalula wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora.

Wito huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo wakati akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo Mkoa wa Tabora.

Kikao hicho kilikuwa ni sehemu ya ziara ya Bodi mkoani humo kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.

Wakili Kalolo ameyasema hayo baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi husika iliyobainisha kuwa baadhi ya Wakandarasi wanasuasua hivyo kuchelewesha kukamilika kwake, jambo lililo kinyume na mikataba yao ya kazi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (kushoto) akizungumza na Mwenyekiti wa Kijiji cha Igalula wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora Athumani Ramadhani, wakati wa ziara ya Bodi hiyo mkoani humo, kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.

Akisisitiza, amesema Serikali kamwe haitamvumilia Mkandarasi yeyote mwenye utendaji kazi duni unaokwamisha miradi hiyo na kuwakosesha wananchi fursa ya kuboresha maisha yao kutokana na nishati ya umeme.

“Kitendo cha kukwamisha kwa kuchelewesha Mradi au kwa namna nyingine yoyote ni uhujumu uchumi. Naomba muelewe Serikali haitakubali hivyo hatutasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekwenda kinyume na Mkataba,” amesisitiza.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mjumbe wa Bodi Oswald Urassa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga walitoa onyo kwa Wakandarasi wanaozembea kuheshimu Serikali ya Tanzania kwani iko thabiti na haina mzaha katika kusimamia miradi ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Katika hatua nyingine, Ujumbe huo wa Bodi ulitembelea maeneo mbalimbali mkoani humo ambako utekelezaji wa miradi ya umeme unaendelea na kuzungumza na viongozi wa vijiji na vitongoji ili kusikia maoni yao.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (katikati) na Ujumbe wake, wakikagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini katika kijiji cha Igalula, wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora wakati wa ziara ya Bodi mkoani humo, Septemba 8, 2021

Akitoa maoni kwa Bodi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Igalula wilayani Uyui, Athumani Ramadhani amesema wananchi katika eneo hilo wameupokea Mradi wa Umeme Vijijini kwa furaha na matumaini.

“Wananchi wameanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mashine za kusaga. Pia tunashukuru maana umeme huu haukatiki-katiki. Ombi langu kwa Serikali wananchi wote wafikishiwe nishati hii,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigwa wilayani Uyui, Hussein Maganga aliishukuru Serikali kwa kubuni miradi ya umeme vijijini akiielezea kuwa imekuwa yenye manufaa makubwa kwa wananchi kwani imechangia kuboresha maisha yao.

Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Oswald Urassa akishuhudia vibarua wa Mkandarasi Kampuni ya Sengerema Engineering Group Limited, anayetekeleza Mradi wa Umeme wa Ujazilizi wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora, wakiendelea na kazi ya kutandaza miundombinu husika katika kijiji cha Kigwa. Bodi ilikuwa katika ziara ya kazi.

Bodi ya Nishati Vijijini inaendelea na ziara katika Mikoa mbalimbali nchini kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.