November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wenye mita za Luku zaidi ya moja watakiwa kuwasilisha taarifa TRA Kilimanjaro

Na Martha Fatael,TimesMajira Online,Moshi

MAMLAKA ya mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro, imetaka wamiliki wa nyumba wenye mita za Luku zaidi ya moja, kuwasilisha taarifa TRA ili itoze Kodi ya jengo katika mita Moja badala ya zote.

Meneja wa TRA mkoani hapa,Masawa Masatu amesema hayo akitoa ufafanuzi wa hoja za wafanyabiashara wa kada tofauti wakipewa elimu kuhusu mabadiliko ya baadhi ya sheria za Kodi nchini.

“Iandikieni TRA mkiainisha mita inayolipa Kodi ya jengo, ili nasi tuielekeze Tanesco ambayo nayo itarejesha fedha ilizokata kimakosa kwa kuwapa Unit za Luku” amesema.

Katika hatua nyingine TRA imeiomba Manispaa ya Moshi, kupanga upya wafanyabiashara ndogondogo (Machinga) ili kuondoa mgongano usio wa lazima na wafanyabiashara wakubwa.

Kauli ya TRA inafuatia hoja ya jumuiya ya wafanyabiashara mkoani hapa, kuwa baadhi ya Machinga Wana mitaji mikubwa ingawa hutumia vitambulisho vya wajasiriamali.

Hata hivyo Masatu ameahidi kufikisha hoja hiyo ngazi za juu za maamuzi ili kutazama kwa kina suala la baadhi ya machinga kujificha katika mgongo wa wafanyabiashara wadogo.

Meneja wa TRA mkoani Kilimanjaro, Masawa Masatu,(aliyesimama), akifafanua Jambo mbele ya wafanyabiashara,hawapo pichani, kulia ni Mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara mkoani hapa, Hillary Lyatuu na kushoto ni meneja madeni na ufuatiliaji wa walipakodi wanaotumia mashine za EFD, Tirson Kabuje

Awali Ofisa elimu na huduma kwa mlipakodi kutoka TRA makao makuu, Lazaro Mafie, amesema utaratibu wa kulipia kodi ya majengo kwa luku umeanza Agosti 20,2021 na itamuhusu mwenye nyumba na sio mpangaji.

Aidha Mafie amesema Kodi hiyo haihusu nyumba za vijijini, nyumba za nyasi na udongo na zile zilizojengwa kwa vifaa visivyodumu.

Amesema jengo la kawaida ni 12,000 kwa mwaka huku ghorofa lililo kwenye mji, manispaa na jiji, kila sakafu inatozwa kwa mwezi Sh 5,000 ili ndani ya mwaka mlipaji awe amelipa Sh 60,000.

Amesema nyumba ya ghorofa zilizopo wilayani, halmashauri na mikoani zitalipa Sh 12,000 kama nyumba za kawaida bila kujali idadi ya sakafu zilizopo katika jengo hilo la ghorofa.

Kuhusu wastaafu, wazee wenye umri kwa zaidi ya miaka 60 wapo kwenye kundi la msamaha Ingawa ni katika nyumba za makazi wanayoishi wenyewe.

Akiwasilisha hoja hiyo, mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara mkoani hapa, Hillary Lyatuu amesema wanahitaji ushindani ulio sahihi kwa wafanyabiashara wote.