Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Masasi
WAZIRI Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Mbunge wa Masasi Mjini, Geoffrey Mwambe kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ameendeleza juhudi zake za kuboresha sekta ya elimu kwa kufanikiwa kugawa kompyuta tano, vifaa vingine kama vile Monitor, extension cable, printer na spika kwa shule za sekondari nne ambazo za Mtandi, Masasi kutwa, Marika na Mtapika zilizopo katika jimbo hilo.
Akizungumza kwa niaba ya Wazir Mwambe, Katibu wa Mbunge huyo, Imani Mkumbo mbali ya kuipongeza Mfuko wa Mawasiliano kwa wote kwa kumuunga mkono mbunge, alisema vifaa hivyo ni miongoni mwa juhudi zinazofanywa na mbunge katika kuhakikisha sekta ya elimu inaimarika jimboni hapo ikiwemo kuzingatia nyakati zilizopo za maendeleo ya sayansi na teknolojia.
“Kwanza ninapenda kuwashukuru wenzetu UCSAF kwa ushirikiano wao, lakini pia wote tunatambua kuwa dunia ya sasa inaende na maendeleo ya sayansi na teknolojia sasa basi hata kwenye elimu pia teknolojia inatumika kwa kiasi kikubwa na imani ya mbunge wetu ni kwamba vifaa hivi vitakwenda kusaidia kwenye kufundishia vijana wetu na hata kutatua changamoto ya uchapaji kazi mbalimbali kwenye shule zetu”, alisema Mkumbo.
Alisema lengo la Mbunge ni kuona na kuhakikisha vijana wengi wakifanikiwa kwenye elimu na kuwataka wanafunzi hao kuvitunza na kuvitumia vifaa hivyo kwa umakini mkubwa ili viweze kutumiwa na wanafunzi wengine wengi zaidi.
“Amenisistiza niwaambie kuwa matamanio yake ni kuona vifaa hivi vikienda kuongeza juhudi zenu kwenye kufanikiwa kwenye masomo yenu lakini pia amewataka muvitunze vifaa hivi ili wenzenu watakaowafata baadae waweze kunufaika navyo”.Alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa shule ya Sekondari ya Marika, Rehema Machemba, akiongea kwa niaba ya wakuu wengine wa shule hizo waliopokea vifaa hivyo, alimshukuru mbunge huyo kwa msaada huo mkubwa ambao unaenda kutatua changamoto za kujifunzia na kuboresha mazingira ya kufundishia katika shule hizo.
“Kipekee ninapenda kumshukuru mbunge wetu sio tu kwa kuttambau umuhimu wa vifaa hivi bali hata kwa kutuletea vifaa hivi ambavyo kwa kiasi kukubwa vitaenda kusaidia sana kwenye kufundishia kwenye shule zetu”, alisema Machemba.
Mwambe tokea kuchaguliwa kwake kuliongoza jimbo hilo, kwa kushirikiana na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Mama Samia Suluhu Hassan na taasisi mbalimbali ameendelea kujikita na kutekeleza kwa vitendo na kuhakikisha jimbo hilo linapiga hatua katika Nyanja muhimu kama vile elimu, maji, afya na miundombinu.
Hivi karibuni Mwambe aligawa magari matatu kwa shule zilizopo katika Wilaya ya Masasi.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu