November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kilimo, ufugaji vyapunguza umasikini kwa asilimia 12

Esther Macha, TimesMajira Online, Mbarali

OFISA Ufuatiliaji wa mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF), Judith Richard amesema kuwa, takwimu zinaonyesha kuwa umasikini wa mahitaji ya msingi kwa kaya za walengwa umepungua kwa asilimia 12 huku mafanikio hayo yakitokana na walengwa kujikita kufanya shughuli mbalimbali kama kilimo, ufugaji, uvuvi na kufanya miradi ya ujasiliamali.

Judith amesema hayo wakati wa kikao kazi cha kuwajengaa uelewa viongozi, watendaji na wawezeshaji kuhusu uandikishaji kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF kwa lengo la kuziwezesha kaya za walengwa wa Mfuko kutumia fursa za kukuza uchumi, kuongeza kipato, kuboresha huduma za jamii na kuendeleza watoto ili kujenga rasilimali watu.

Amesema, maeneo yote ambayo hayakufikiwa katika awamu zilizopita yatafikiwa katika kipindi hiki kwa pande zote mbili za Muungango na zile zitakazokidhi vigezo zitaandikishwa katika daftari la walengwa wa TASAF.

Katika kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF kinatekelezwa katika Halmashauri 184 za Tanzania bara na Wilaya zote za Zanzibar ambapo wameweza kuzifikia Kaya 1,450,000 zenye watu milioni 7.

Akifungua kikao kazi, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Rubeun Mfune amesema, kikao hicho cha kuwajengea uelewa viongozi, watendaji na wawezeshaji kuhusu uandikishaji kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF kwa lengo la kuziwezesha kaya za walengwa wa Mfuko kutumia fursa za kukuza uchumi, kuongeza kipato, kuboresha huduma za jamii na kuendeleza watoto ili kujenga rasilimali watu.

“Nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza dhamira ya nchi yetu ya kupunguza umasikini na kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii ambazo ni pamoja na elimu afya na maji kwa kushirikisha jamii na kukuza dhana ya kujitegemea,”.

“Tulikuwa tunaulizwa na wananchi kuwa ni lini vijiji ambavyo havikuwa kwenye mpango wa TASAF vitahudumiwa na Serikali, nawaomba madiwani muwaeleze wananchi kuwa Serikali imesikia kilio chao, Vijiji ambavyo havikuwa kwenye mpango vinaandikishwa na vitaendelea kuhudumiwa kuanzia mwaka huu wa fedha”.

“Viongozi wenzangu ambao mmejengewa uelewa mkawe mabalozi wa kuzungumzia TASAF katika maeneo yenu na kuwaelekeza wananchi madhumuni ya TASAF na nini wajibu wao katika kuhakikisha wanatoka kwenye hali duni na kujikwamua kiuchumi,”. amesema Mfune.

Amesema kuwa, kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF kinatekelezwa katika Halmashauri 184 za Tanzania bara na Wilaya zote za Zanzibar ambapo kimeweza kuzifikia kaya 1,450,000 zenye watu milioni 7.

Akiongea kwa niaba ya Madiwani wa Halmashauri hiyo, Makamu Mwenyekiti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Chuki Mbwanjine ameishukuru Serikali kwa kuwa sikivu na kuviingiza vijiji vyote kwenye mpango wa TASAF kwani siku zote wamekuwa wakiulizwa na wananchi kuhusiana na vijiji ambavyo havikuingizwa kwenye mpango, wameahidi kuwa mabalozi wazuri kwa wananchi.