Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Dar es Salaam
SHIRIKA la Legal Services Facility (LSF) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo imezindua mradi utakaowawezesha wananawake wanaomiliki vipande vya ardhi katika wilaya hiyo kupata hati za umiliki wa ardhi zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi na pia kupata elimu juu ya masuala ya ardhi.
Mradi huu ujulikanao kama; “Hati yangu maisha yangu” umeanzishwa mahususi ili kukabiliana na changamoto zinazowakumba wanawake wa hali ya chini, ambao wanamiliki ardhi lakini wameshindwa kukamilisha zoezi la umilikishwaji kutokana na kutoweza kumudu gharama zitokanazo na upatikanaji wa hati.
Aidha mradi huu pia umelenga kutoa elimu kwa wanananchi juu ya sheria za ardhi, umilikishwaji ardhi, haki ya kurithi na kumiliki ardhi ili kuongeza uelewa na kupunguza changamoto zinawaathiri wanawake kwa sasa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huu, Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala alisema;
“Tunayo furaha kubwa kubuni mradi huu na kutoa ruzuku kwa TAWLA kuutekeleza kwa lengo la kuboresha maisha ya wanawake na kusaidia kupunguza umaskini.
LSF tunatambua wanawake wanapitia changamoto nyingi sana zikiwemo unyanyasaji wa kijinsia, kutopata fursa sawa katika masuala ya kiuchumi , kiuongozi, lakini pia wamekuwa na majukumu mazito katika kulea na kuhakikisha ustawi wa familia zao. Hivyo tunaamini kupitia mradi huu tutawawezesha kumiliki ardhi walizonazo na kuzitumia katika kupata mitaji na kukuza shughuli zao za kiuchumi kwa manufaa ya familia zao na taifa kwa ujumla.
Alisema kupitia mradi huu wataweza kuwafikia wanawake 2,000 kwa kuwapatia elimu na zaidi ya wanawake 300 watapata hati miliki zao kwa kuchangia gharama kidogo sana.
Aliongeza kwamba LSF imejipanga kuchangia gharama za urasimishaji na upatikanaji wa hati kwa asilimia 80 na mwananchi atatakiwa kuchangia asilimia 20 tu. Hii ni nafasi ya kipekee kwa wanawake wanaoishi katika wilaya ya Ubungo kunufaika kwa kuchangamkia fursa hii. Alisisitiza Ng’wanakilala
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ubongo, Beatrice Dominuo Kwai, alitoa shukrani zake za dhati kwa TAWLA ambao ni watekelezaji wa program pamoja na LSF ambao ni wafadhili wa program hii, kwa kuweza kutambua changamoto zinazowakabili wanawake katika jamii na kuamua kuchagua kutekeleza program hii katika Halmashauri ya Ubungo.
“Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwepo kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa kudhibiti na kuzuia makazi yasiyopangwa (2012-2021) katika maeneo ya miji na mijini.
Dar es Salaam ikiwa ni moja ya mikoa inayonufaika na mpango huo hususani katika Wilaya ya Ubungo,”alisema.
‘Ni matumaini yetu kupitia programu ya Hati yangu maisha yangu itasaidia kuwawezesha wanawake hususani wasiojiweza katika kata ya Mbezi, Msigani, Kwembe, Goba na Kibamba kuweza kupimiwa maeneo yao kwa kuchangia gharama za upimaji.Vile vile tunaamaini kupitia elimu itakayotolewa kwa jamii itasaidia kubadilisha dhana potofu juu ya haki za wanawake katika kumiliki ardhi pamoja na kuongeza uelewa kwa wanawake katika masuala ya umiliki wa ardhi na jinsi ya kutumia ardhi kama vyanzo vya uchumi.
Kwani ni ukweli usiopingika kuwa dhana hizi potofu zimeleta athari kwa wanawake walio wengi na kusababisha kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia katika kumiliki ardhi.
Nitoe rai kwa wanawake kutoka kata husika wajitokeze kwa wingi ili waweze kupata elimu juu ya haki zao katika kumiliki ardhi na fursa za kiuchumi pamoja na kupimiwa maeneo yao ambayo kikwazo kilikuwa ni gharama za upimaji”. Aliongeza Kwai.
Naye Mkurugenzi Mkuu TAWLA, Tike Mwambipile alisema “TAWLA chini ya ufadhili wa LSF kwa kuthamini mchakato wa urasimishaji wa ardhi unaoendelea hivi sasa nchini Tanzania na kuhakikisha ulinzi wa haki za wanawake katika kumiliki ardhi itafanya kazi kwa karibu sana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo ili kufanikisha wanawake pamoja na makundi maalum kupimiwa ardhi na kupatiwa hati miliki, kuongeza uelewa kwa wanawake katika masuala ya umiliki wa ardhi na jinsi ya kutumia ardhi kama vyanzo vya uchumi, kutoa elimu kwa viongozi katika ngazi za kata na mitaa, viongozi wa dini na wasaidizi wa kisheria juu ya wajibu wao wa kulinda haki za wanawake na kuwezesha wanawake kupata hati miliki pamoja na kutoa elimu juu ya fursa mbalimbali za kiuchumi ili kuimarisha uchumi kwa wanawake na familia zao.”
Mradi huu wa Hati yangu maisha yangu umezinduliwa katika wilaya ya Ubungo ikiwa ni sehemu ya majaribio, lakini lengo ni kuutekeleza nchi nzima.
Ili kunufaika na mradi huu wanawake kutoka katika kata za Mbezi, Goba, Kwembe, Kibamba na Msigani watatakiwa kushiriki wakati wa zoezi zima litakapoanza, zoezi hili litawalenga wanawake wenye uwezo mdogo ambao wanamiliki vipande vya ardhi, lakini wameshindwa kupata hatamiliki kwa sababu ya gharama za upatikanaji wa hatimiliki.
More Stories
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania