Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Dar
CHUO Kikuu cha CT kilichoko katika mji wa Punjab nchini India kimetoa ufadhili wa nusu ada kwa wanafunzi 100 Watanzania wanaotaka kusomea ufamasia kwenye chuo hicho.
Ofa hiyo imetangazwa wiki hii na Mkurugenzi wa Idara ya Kimataifa ya chuo hicho, Sourabh Chaudhary.
Alikuwa akizungumza na wanafunzi na watu mbalimbali wanaotembelea maonesho ya vyuo vikuu yanayoendekea kwenye viwanja vya Mnazimmoja jijini Dar es Salaam.
Chuo hicho na vingine tisa vimekuja nchini kuonesha kozi wanazotoa kwenye maonesho hayo kwa mwamvuli wa wakala mkubwa wa elimu nje ya nchi, Global Education Link (GEL).
Amesema wanafunzi wote 100 watakaopenda kusoma fani hiyo kwenye chuo hicho watapata punguzo Maalum (Scholarship) hadi asilimia 50 na utaratibu wa safari utakuwa mwezi huu wa nane.
Alisema kwa wanafunzi ambao bado wako kwenye mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wao wataingia chuoni kuanzia mwezi wa Tisa.
Sourabh amesema urafiki kati ya Tanzania na India ni wa miaka mingi na kwamba Serikali ya Tanzania imewekeza kwa kiasi kikubwa sana katika sekta ya afya, hivyo ni dhahiri inahitaji wataalamu wa kutosha kuhudumia sekta hiyo.
Amesema pia Serikali ya Tanzania imejitahidi kuboresha miundombinu kwa wanafunzi wa sayansi wakiwepo hao wanaotaka kusoma kozi za afya.
“Kwa kutumia urafiki baina ya nchi hizi mbili uongozi wa chuo umekubaliana ni vyema kuchagua kozi ambayo ina umuhimu na uhitaji mkubwa katika soko la ajira kwa kuipunguzia gharama ili Watanzania wengi waweze kuisoma kwa maendeleo ya nchi na taifa kwa ujumla,” alisema
Amewahakikishia wazazi kwamba wanafunzi kutoka Tanzania huwa wanafanya vizuri sana kutokana na maandalizi mazuri yao katika elimu ya sekondari na wengi wao hupokea tuzo mbalimbali kutokana na umahiri wao wa kufanya vizuri,kujishirikisha na michezo na kuonesha tabia njema wawapo chuoni.
Amesema mbali na kozi hiyo ya famasia zipo kozi nyingi akitaja baadhi kuwa ni uhandisi, sanaaa na paramedics na artificial intelligence kwa uchache.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato