November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wapongeza kauli ya Masauni kuitaka Benki Kuu kupunguza viwango vya riba

Na Suleiman Abeid,TimesMajira Online,Shinyanga

BAADHI ya wamiliki wa makampuni yanayotoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo mjini Shinyanga wameipongeza kauli ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Masauni kuitaka Benki Kuu ya Tanzania kupunguza viwango vya riba zake.

Wakizungumza na waandishi wa habari juzi mjini Shinyanga wamiliki hao wamesema pamoja na pongezi zao kwa waziri lakini pia wameomba kampuni zao ziruhusiwe kukopa moja kwa moja kutoka Benki Kuu badala ya utaratibu wa sasa wa kukopeshwa na baadhi ya Taasisi za kifedha.

aibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Bernard Kibesse, akifafanua jambo wakati wa mkutano kati ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb) (hayupo pichani) na Viongozi wa BoT wakiwemo Manaibu Gavana na Wakurugenzi, jijini Dar es Salaam.

Wamesema kwa mujibu wa taratibu zilizopo hivi sasa makampuni yao yanakopeshwa fedha na Taasisi ya kifedha ya Self Microfinance ambayo hata hivyo haina uwezo wa kukopesha kiwango kikubwa cha fedha kama ambavyo Benki Kuu ingetoa.

Mmoja wa wamiliki wa makampuni hayo mjini Shinyanga, Julius Ntiga amesema baada ya Serikali kufungua milango kwa kampuni binafsi kuendesha shughuli za utoaji mikopo kwa wananchi mbalimbali watu wengi wamejitokeza kuomba kukopeshwa.

Hata hivyo Ntiga alisema pamoja na kuwepo kwa fursa hiyo bado wanakabiliwa na changamoto ya gharama za uendeshaji kuwa kubwa na kujikuta wakijiendesha kwa hasara kutokana na sheria ama kanuni za riba kuwabana wakitakiwa kutoza riba kidogo kiwango cha asilimia 3.5.

“Tunampongeza Naibu Waziri wetu wa fedha kwa kuitaka Benki Kuu kupunguza viwango vyake vya riba, lakini pamoja na pongezi hizi tunafikiri ni wakati muafaka kwa Serikali na Taasisi zetu kuwa na kikao cha pamoja kuangalia jinsi gani tutatekeleza jukumu tulilonalo bila ya sisi kupata hasara,”

“Mpaka hivi sasa tunafanya shughuli zetu kihasara japo tuna mchango mkubwa katika kumsaidia Mtanzania mwenye kipato cha chini ambaye hakidhi vigezo vya kukopeshwa na mabenki makubwa ya kibiashara, changamoto hii ni kiwango cha riba ya mkopo asilimia 3.5 tunayotakiwa kuwatoza wateja wetu,” ameeleza Ntiga.

Akifafanua amesema kiwango cha riba wanachopaswa kuwatoza wateja wao hakikidhi kurejesha gharama zote za uendeshaji ambapo pia hata idadi ya wateja wao ni wachache ikilinganishwa na wanaokopa kwenye mabenki makubwa.

Mmiliki mwingine wa Kampuni ya Msilikare Microfinance, Robert Manyanyiho alisema iwapo Serikali italegeza masharti yake na wao kuruhusiwa kukopa moja kwa moja kutoka Benki Kuu wanaweza kuwa nafuu na hivyo kupata uwezo wa kuwasaidia wajasiriamali wengi wadogo.

“Ni kweli benki za kibiashara zinatoza riba za chini lakini hii ni kwa vile wao wana wateja wengi na wenye uwezo mkubwa wa kifedha ikilinganishwa na wateja wetu ambao ni wajasariamali wadogo na hawakidhi vigezo vya kukopeshwa na mabenki makubwa, hivyo tegemeo lao ni kwetu,” ameeleza Manyanyiho.

Manyanyiho amesema kuna umuhimu wa Serikali kuangalia uwezekano wa wao kuongeza kidogo kiwango cha riba wanachowatoza wateja wao ili kiweze kurejesha gharama za uendeshaji ikiwemo ulipaji mishahara wafanyakazi na pango za kila mwezi za ofisi.

Pongezi za wamiliki wa makampuni hayo zimeungwa mkono na baadhi ya wajasiriamali wadogo wanaoendesha biashara zao mjini Shinyanga ambapo walisema iwapo wataruhusiwa na Serikali kukopa moja kwa moja kutoka Benki Kuu huenda riba wanayotoza hivi sasa ikatosheleza kukidhi gharama zao za uendeshaji.

Mmoja wa wajasiriamali hao, Mary James mkazi wa kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga anayejishughulisha na utengenezaji wa nguo za batiki alisema hivi sasa wajasiriamali wengi wanategemea zaidi mikopo kutoka kwa Taasisi binafsi kutokana na kutokuwa na vigezo vya kukopeshwa na benki kubwa.

“Tumesikia Naibu waziri wa Fedha akiitaka Benki Kuu kupunguza riba zake, ni vizuri, lakini sisi tunaiomba Serikali hii ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Hassan Suluhu iangalie uwezekano wa kuyasaidia makampuni binafsi yanayotoa mikopo kwa wajasiriamali yaweze kuwa na mitaji mikubwa,” ameeleza Mary.

Mwisho.