November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kwimba wajitokeza kupata elimu kuhusu mradi wa SGR

Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza

WANANCHI wa Kata ya Malya,Mwandu na Mantale wilayani Kwimba pamoja na Ukiriguru, Mamaye na Kolomije za wilayani Misungwi,mkoani Mwanza wamejitokeza kwa wingi katika kampeni ya uelewa kuhusu mradi wa kipande cha tano cha reli ya kisasa (SGR) Mwanza-Isaka yenye kilomita 341.

Mtaalamu kutoka katika Kitengo cha Ulinzi na Usalama Wa Reli TRC, Mussa Mhagama, akionesha moja kati ya alama za tahadhari zitakazowekwa katika eneo la mradi, wakati wa kampeni ya uelewa wa jamii kuhusu mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa SGR Mwanza – Isaka, kijiji cha Ibogoya “A” Kata ya Kolomije, wilayani Misungwi Mkoani Mwanza.picha na Judith Ferdinand

Huku wakieleza namna elimu hiyo inayotolewa na wataalamu kutoka shirika la Reli Tanzania(TRC),vitengo vya Uhandisi, Ardhi, Habari na Mawasiliano, Mazingira, Ulinzi na Usalama wa Reli pamoja na Kitengo cha Masuala ya kijamii,itakavyowasaidia hasa vijana, kutambua na kuzifanyia kazi fursa za kimaendeleo zinazotokana na mradi huo.

TRC inaendelea na kampeni maalum ya utoaji wa elimu juu ya ujenzi wa reli ya kisasa, awamu ya kwanza kipande cha tano, Mwanza – Isaka (km 341), kwa jamii zinazoishi maeneo yatakayopitiwa na mradi huo.

Wakizungumza katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika kata hizo, wananchi wameelezea jinsi ambavyo wameipokea kampeni ya Uelewa kuhusu mradi huo wa Kimkakati na kihistoria kwa taifa.

Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Kitunga, Kata ya Malya wilayani Kwimba,Mathias Nyama,amesema elimu hiyo walioipata kutoka kwa wataalamu wa TRC itawasaidia kutambua hasa wao vijana,maana fursa za kujikwamua kiuchumi zipo nyingi huku akiahidi kuwa wataulinda mradi.

Naye mwananchi wa kijiji cha Magaka, Kata ya Mamaye Wilayani Misungwi Neema Joseph,amesema kupita kwa mradi huo utawanufaisha wakazi wote walio karibu na mradi huku akiiishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati unaolenga kuwanufaisha Watanzania na taifa.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR Mwanza – Isaka, Mhandisi Mchibya Masanja, ameeleza kuwa lengo la kampeni hiyo ya uelewa kuhusu mradi wa ujenzi wa SGR Mwanza – Isaka,ni kuhakikisha uelewa sahihi wa masuala yanayohusiana na mradi kwa viongozi na wananchi kwa ujumla ili kufikia maendeleo ambapo ni moja kati ya hatua muhimu za awali za utekelezaji wa mradi.

Afisa Mwandamizi, Kitengo cha Ardhi TRC, Fredrick Kusekwa,akizungumzia masuala ya uthamini na fidia katika mkutano wa kampeni ya uelewa wa jamii kuhusu mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa SGR, uliofanyika katika Kijiji cha Fela wilayani Misungwi, Mkoani Mwanza.picha na Judith Ferdinand

“Mradi huu ni shirikishi, kwaio tunafanya kampeni hii ili kuhakikisha mradi unakuwa na tija kwa wananchi ambao ndio walipakodi na fedha zao zinazotumika katika utekelezaji huu,tunataka mradi ubadilishe maisha ya watu kwa kuwaletea maendeleo,”amesema Mhandisi Machibya wakati akitoa ufafanuzi wa kampeni hiyo katika moja ya mikutano ya hadhara iliofanyika katika kata hizo.

Amesema pia katika kampeni hiyo inategemea kuwafikia viongozi na wananchi wa Mikoa ya Simiyu na Shinyanga ambayo pia inapitiwa na kipande cha tano cha Ujenzi wa Reli ya Kisasa (Mwanza – Isaka) kinachogharimu kiasi cha trilioni 3.

Mtaalamu kutoka katika Kitengo cha Ulinzi na Usalama wa Reli TRC, Mussa Mhagama, ametoa elimu pamoja na kuwaonesha wananchi alama za tahadhari zitakazowekwa katika eneo la mradi,ili waseweze kukumbwa na madhara yoyote wakati utekelezaji ukiendelea.

Hata hivyo Ofisa Mwandamizi, Kitengo cha Ardhi TRC,Fredrick Kusekwa amewaeleza wananchi juu ya masuala ya uthamini na fidia itakavyokuwa ambapo awali akizindua rasmi kampeni hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi, aliwahakikishia Wanamwanza na Kanda ya Ziwa, kuwa wananchi wote watakaopitiwa na mradi huo watalipwa stahiki zao kwa mujibu wa sheria.