November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yadhamiria kwenda kidigitali

Na Zena Mohamed,TimesMajira Online

IMEELEZWA kuwa kutokana na maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Tanzania inakwenda kwenye uchumi wa kijiditali ambapo kwa sasa vitu vingi hasa bili za maji, luku na malipo ya ardhi yanafanyika kwa njia ya mtandado.

Hayo yameelezwa jijini hapa leo na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Dkt.Faustine Ndugulile wakati akizindua tovuti ya wizara hiyo na mpango mkakati wa wizara wa miaka mitano kwenye hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete.

Dkt.Ndugulile amesema, wako katika kuiandaa Tanzania kwenda kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda.

“Mwelekeo wa wizara hiyo ni kuwafanya Watanzania wote wawe katika uchumi wa kidijitali kwa kufanya biashara zao kwenye mtandao,”amesema.

Aidha, amesema uchumi wa kidijitali unaondoa biashara ya fremu za maduka kwa kuwa muuzaji hatakuwa na haja ya kuweka bidhaa zake dukani na badala yake atauza kwenye mtandao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt.Zainab Chaula amesema, wizara hiyo imejipanga kuongeza mfumo wa mawasiliano na kuachana na utaratibu wa kila wizara kuwa na mfumo wake wa mawasiliano.

Amesema, hata Rais Samia Suluhu Hassan alishangazwa na kila wizara kuwa na mfumo wake na kutaka mfumo wa uwe mmoja kwa ajili ya kuongeza ufanisi.

Pia Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso amesema, wabunge wako pamoja na wizara hiyo na aliomba iboreshe TTCL ili iweze kusimama na kutoa gawio kwa Serikali.