Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dar
MCHANGO wa wazalishaji, waagizaji na wasambazaji wa mifuko ya Non Woven na ile ya plastiki katika pato la taifa na upatikanaji wa ajira utatokana na wao kuzalisha mifuko yenye kukubalika katika masoko, yenye ubora inayokidhi matakwa ya viwango husika.
Hayo yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Lazaro Mwambole, wakati akifungua mafunzo ya wazalishaji, waagizaji na wasambazaji wa mifuko ya Non Woven na ile ya plastiki kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Dkt. Yusuf Ngenya, jijini Dar es Salaam juzi.
Amesema TBS kwa kuunga mkono mipango na juhudi zote zinazofanywa na Serikali katika kukuza pato na kuongeza ajira kupitia sekta hiyo, ndiyo maana imekuwa ikitumia mamlaka iliyopewa ili kuhakikisha kuwa, bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa hapa nchini ni zile zinazozalishwa nchini ikiwemo mifuko ya Non-woven bags, mifuko ya plastiki iliyoruhusiwa na sacks bags zinakidhi matakwa ya viwango.
“Kwa mantiki hiyo TBS itaendelea kutilia mkazo kusimamia masuala ya viwango na udhibiti ubora wa bidhaa,” amesema Mwambole.
Amesisitiza kwamba lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha biashara za vifungashio zinafanywa katika mifumo inayoeleweka na kukubalika kisheria sambamba na kanuni zinazosimamia mifumo ya viwango na udhibiti ubora.
Amesema hatua hiyo inalenga kuzingatia sheria zinazosimamia mazingira dhidi ya uchafuzi unaotokana na bidhaa za vifungashio baada ya matumizi yake.
Kwa msingi huo, Mwambole amesema mafunzo haya yanalenga kuandaa washiriki kuwa wenye mwelekeo mzuri zaidi na wa kiuweledi katika kuzalisha, kuingiza na kusambaza non-woven bags, mifuko ya plastiki iliyoruhusiwa na sacks bags zinazokidhi matakwa ya viwango.
“Hii inatokana na ukweli kwamba sio watu wote wanaweza kushiriki katika sekta hii ya biashara. Mara nyingi watumiaji hutegemea sana wasambazaji,” amesema Mwambole na kuongeza;
“Hivyo, wawashauri juu ya aina na ubora wa bidhaa wanazozihitaji sokoni, ikiwa mtumiaji hawezi kupata bidhaa yenye ubora na inayoendana na mahitaji yake husababisha kuwepo kwa malalamiko juu ya thamani ya maisha yao na fedha zao.”
Wakizungumzia mafunzo hayo, baadhi ya washiriki wamesema mafunzo ya namna hiyo yamekuja wakati muafaka ambapo Serikali ya Awamu ya sita imeazimia kwa dhati kabisa kuwekeza na kuendeleza viwanda ili kutoa ajira katika kada mbalimbali pamoja na kuziwezesha bidhaa zetu kushindana katika masoko ya ndani, kikanda na nje ya Tanzania.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Rashid Abdallah amesema mafunzo haya ni uthibitisho wa azma ya Serikali kupitia taasisi zake katika kufanikisha malengo ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kwa hilo wanaona muelekeo mzuri chini ya usimamizi wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Kwenye mafunzo haya wawezeshaji kutoka TBS walitoa mada kuhusu viwango na matakwa ya viwango vya Non-woven bags, sacks bag na mifuko mingine ya plastiki iliyoruhusiwa kisheria.
Mada hizo zilijikita katika kutoa ufafanuzi wa kina juu ya matakwa ya viwango kama yalivyoainishwa kwenye viwango vya kitaifa. Viwango hivyo ni TZS 1726: 2015, TZS 1729: 2015, TZS1730: 2015, FTZS 1257: 2021, TZS na FTZS 2709: 2021.
More Stories
TARURA Kilimanjaro yatimiza ahadi ya Rais Samia
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria
Wananchi wakubali yaishe Bangi kubaki historia Tarime