Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Dar
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limekabidhi maabara mbili zinazotembea na mashine mbili kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kwa ajili ya kutambua vinasaba kwenye mafuta yanayouzwa katika soko la ndani, hasa kwenye vituo vya mafuta.
Hafla ya makabidhiano ya maabara hizo ilifanyika jijini Dar es Salaam jana na kushuhudiwa na maofisa wa TBS na EWURA.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Mkuu wa Shughuli za Uwekaji Vinasaba wa TBS, Mhandisi Frolian Batakanwa, amesema maabara hizo pamoja na mashine mbili zitafanyakazi na kama ikitokea mashine mmoja ikaharibika, nyingine itafanyakazi ili kuhakikisha kazi inafanyika kwa ufasaha zaidi.
Amesema shirika hilo lilianza utaratibu wa kutambua kiasi cha vinasaba kwenye mafuta hasa kwenye soko la ndani pale TBS ilipoanza kuweka vinasaba kwenye mafuta, hivyo hatua hiyo ni mwendelezo wa kuipatia EWURA vifaa ambavyo itavitumia kwenye kazi zake.
“Kwa hiyo kwenye masoko hapa nchini tuna magari yenye maabara kwa ajili ya kutambua vinasaba na hiyo itatusaidia kujua mafuta ambayo hayakidhi ubora au yamechanganywa na mafuta mengine,” amefafanua Batakanwa.
Kwa mujibu wa Batakanwa, maabara hizo zinazotembea na ndani kuna mashine kwa ajili ya kufanya utambuzi, kompyuta ya kuendesha mashine pamoja na vifaa vingine.
“Kwa hiyo tunaomba Watanzania watambue kwamba hatua hiyo ni endelevu, kwani ukiweka vinasaba kwenye mafuta lazima uwe na teknolojia ya kuweza kutambua kama vimewekwa kwa kiasi kinachotakiwa na watu gani sokoni wana mafuta ambayo hayana vinasaba,” amesema Batakanwa
Kwa hatua hiyo, Batakanwa amesema Watanzania watarajie shughuli ya uwekaji vinasaba na kutambua kama vipo kwa usahihi kwenye mafuta itafanyika kwa ufasaha wa hali ya juu.
“Kwa hiyo kwenye taasisi zetu (TBS na EWURA) kila moja kwa kufuata sheria iliyoweka taasisi hizo itafanyakazi zake sawia kulingana na upatikanaji wa maabara hizi zinazotembea,” amesema Batakanwa na kuongeza kwamba mbeleni wataendelea kuongeza ufanisi kwa kuongeza maabara na mashine zingine.
Amesema TBS inafanyakazi ya kuweka vinasaba kwenye mafuta, hivyo lazima ihakikishe kinasaba kinachowekwa kipo kwenye ubora wa kiwango kinachohitajika.
“Kwa hiyo pale makao makuu ya shirika tuna maabara ya Uthibiti Ubora kazi yake ni kuangalia hicho kinasaba kama kinafikia kiwango kinachotakiwa.
Hizi maabara zinazotembea zimekuja kwa ajili ya kusaidia EWURA iweze kufanyakazi zake vizuri sokoni kwa kujibu wa sheria,” amesema Batakanwa.
Kwa upande wake Meneja Ufundi wa EWURA, Mhandisi Shaban Seleman akizungumza baada ya kupokea maabara hizo amesema wao kama wasimamizi wa ubora wa mafuta yanayosambazwa nchini watatumia maabara hizo kuhakikisha mafuta yote yanayosambazwa nchini yanakidhi viwango vya ubora ili kutoharibu magari na mitambo mingine inayotumia mafuta.
“Maabara hizi zitatusaidia kuhakikisha biashara ya mafuta inafanyike kwa uhalali, wasiwepo wafanyabiashara wajanja ambao wanatumia mafuta ambayo hayajalipiwa kodi kwa kuyaingizwa kwenye soko kwa lengo la kuua biashara za watu wengine,” amesema Shaban. Alisema vifaa hivyo vitawaidia kuendelea kusimamia jukumu lao.
More Stories
TARURA Kilimanjaro yatimiza ahadi ya Rais Samia
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria
Wananchi wakubali yaishe Bangi kubaki historia Tarime