November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Gomes atuma salamu Yanga

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

USHINDI wa goli 1-0 walioupata Simba dhidi ya Azam na kufanikiwa kutinga hatua ya fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam ‘Azam Sports Federation Cup (ASFC)’ umezidi kuwapa kiburi benchi la ufundi la timu hiyo ambalo limeapa kubeba alama zote tatu katika mchezo wao wa kiporo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) wa Julai 3.

Katika mchezo huo goli pekee lilifungwa dakika ya 89 na Luis Miquissone aliyemalizia pasi mpira wa adhabu uliopigwa na Benard Morrison aliyeanza haraka mpira huo baada ya kufanyiwa madhambi na beki wa Azam, Bruce Kangwa nje kidogo ya mstari wa 18.

Simba itaingia katika mchezo huo huku ikiwa imeweka rekodi ya kushinda mechi zao tano mfululizo baada ya kuwafunga 3-0 Kaizer Chiefs, 3-1 dhidi ya Namungo, waliibuka na ushindi wa goli 3-0 dhidi ya ruvu shooting, 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania, 4-1 na Mbeya City huku juzi kuwafunga Azam 1-0.

Baada ya mchezo huo sasa vita kubwa ipo kwa Simba na Yanga ambao wanachokihitaji ni kila mmoja kuendeleza ubabe kwa mwenzake baada ya kulazimishana sare ya goli 1-1 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Januari 13.

Kocha mkuu wa klabu ya Simba, Didier Gomes Da Rosa amesema, amefurahishwa na upambanaji wa wachezaji wake ambao wameiwezesha timu kutinga fainali n ani kama zawadi kwa mashambiki wao ambao watashuhudia dabi nyingine ukiacha ile ya Julai 3.

Amesema, kama timu wana ujasiri wa kutosha, nguvu na morali ya kufanya vizuri licha ya kutambua ugumu ulio mbele yao lakini ni lazima watimize mkakati wao wa kutwaa mataji yote ya msimu huu na kama wataendeleza rekodi yao ya kutokufungwa basi jambo la kutimika mikakati yao lipo jirani.

“Ushindi wa mechi sita mfululizo katika mechi za michuano mbalimbali umetuongezea morali ya kuanza maandalizi kuelekea katika mchezo wetu ujao kwani tunachokihitaji ni ushindi na tukifanikiwa kwenye hili basi ubingwa utakuwa wetu,” amesema Gomes.

Kuelekea katika maandalizi ya mchezo huo kocha huyo amesema, wapo wachezaji atakaowakabidhi majukumu maalum kwani anaamini wataweza kuisukuma timu kupata matokeo bora anayoyahitahi na kutangaza ubingwa kupitia mchezo huo.

Gomes amesema kuwa, mchezo wao dhidi ya Yanga utakuwa na tofauti kubwa na ule uliopita dhidi ya Azam kwani anatambua ushindani mkubwa uliopo katika mchezo huo wa ‘Kariakoo Derby’ na kwakuwa walitoka sare katika mchezo uliopita basi wanajipanga kushinda mchezo huo.

“Nishaona mechi kadhaa za Simba na Yanga na jinsi ushindani unavyokuwa, hivyo kazi kubwa iliyo mbele yetu ni kwenda kujiimarisha ili kuwa bora zaidi na kuweza kupata ushidhi ambao utatufanya kutangazwa kuwa mabingwa wapya msimu huu,” amesema kocha huyo.