Kifo chake chatokea ghafla, ni mbunge wa pili mwezi huu, Rais Magufuli, Spika, wabunge wamlilia, mazishi yake kufanyika leo
Doreen Aloyce na Joyce Kasiki, Dodoma
MBUNGE Jimbo la Sumve kwa tiketi ya CCM, Richard Ndassa, amefariki jijini Dodoma alipokuwa kwa ajili ya kuhudhuria vikao vya Bunge la Bajeti linaloendelea mkoani humo.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, alithibitisha kutokea kifo cha Mbunge Ndassa kilichotokea ghafla jana na kuahirisha kikao cha Bunge ili kutoa nafasi kwa wabunge kuomboleza kifo chake.
Ndasa ni mbunge wa pili kufariki katika kipindi cha mwezi huu, ambapo hivi karibuni Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya CCM na Mchungaji wa Kanisa la Mlima wa Moto, Mchungaji Getrude Rwakatare, alifariki na mazishi yake kusimamiwa na Serikali yakihudhuriwa na watu wasiozidi 10.
Akiahirisha kikao cha Bunge jana, Spika Ndugai alisema Bunge limepata pigo lingine kubwa na kwamba kikao kitaendelea kesho (leo) ili kutoa nafasi kwa wabunge kuomboleza kifo cha mbunge mwenzao.
Alisema kwamba kufuatia msiba huo taratibu mbalimbali zimeanza kufanyika kati ya ofisi yake, familia kwa kushirikiana na Serikali.
Marehemu Ndassa ni kati ya wabunge waandamizi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo aliingia bungeni mwaka 1995, akiongoza Jimbo la Sumve kwa vipindi vitano mfululizo ikiwa ni takribani miaka 25.
Tangu akiwa mbunge Ndasa amekuwa chachu muhimu katika Bunge, jambo ambalo lilipelekea kuaminiwa na wananchi. Kufuatia utendaji wake huo, Spika Ndugai aliwataka wabunge kufuata nyayo zake.
Katika hatua nyingine, Spika Ndugai alisema kufuatia mila za kiafrika watajitahidi kwa kushirikiana na Serikali ili marehemu Ndassa azikwe leo jimboni kwake Sumve.
Kuwa upande wao wabunge wakizungumza kwa nyakati tofauti, walielezea kusikitishwa na kifo hicho na wengine kuonekana kutawaliwa na simanzi kutokana na kifo cha mbunge mwenzao kuwa ni cha pili katika kipindi kifupi.
Mbunge Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Rita Kabati, alisema walikuwa wote na marehemu wiki iliyopita Bungeni na alitoa mchango wake kwa baadhi ya wizara.
“Wabunge walizoea kumuita seneta kutokana na uzoefu wake na aliwashauri wabunge katika nyanja mbalimbali,” alisema Kabati.
Naye mbunge viti maalum Mkoa wa Pwani, Zaynab Matitu alisema marehemu walikuwa wote kwenye Kamati ya Watu Tisa kwa ajili ya kufanya kazi za chama ambapo walishirikiana na kazi waliimaliza vizuri.
Alisema kutokana na ushirikiano huo ilionyesha ni kiasi gani marehemu alijali na kutetea maslahi ya Watanzania na wananchi wake jimboni
Wakati huo huo, Rais John Magufuli, ametuma salamu za rambirambi kwa familia, Spika wa Bunge, Job Ndugai na wananchi wa Jimbo la Sumve Mkoani Mwanza kufuatia kifo cha Mbunge wa Jimbo hilo, Richard Ndassa.
Rais Magufuli alisema; “Nimesikitishwa na taarifa za kifo cha ghafla cha Ndassa, nakumbuka mimi na yeye tulianza pamoja Ubunge mwaka 1995, yeye akiwa Mbunge wa Jimbo la Sumve na mimi nikiwa mbunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki ambalo sasa hivi linaitwa Jimbo la Chato, namuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina.”
Rais Magufuli amemuomba Spika Ndugai kufikisha salamu zake za pole kwa familia ya marehemu, wabunge, wananchi wa Sumve pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na kifo cha Ndassa.
Aliwataka wafiwa wote wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi ya kuondokewa na mpendwa wao.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa