Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
BAADA ya kikosi cha timu ya Taifa ya Wavu Ufukweni (Beach Volleyball) kushindwa kwenda nchini Morocco kwa ajili ya michuano ya Kombe la Afrika ambayo pia itatumika kwa ajili ya kusaka tiketi ya kushiriki michuano ya Olimpiki ‘Africa Sub Zonal V Olympic Qualifiers’, itakayofanyika Tokyo, Japan kuanzia Julai 23 hadi Agosti 8, 2021, Chama Cha Mpira wa Wavu Tanzania (TAVA) sasa kimehamishia mikakati yake katika michuano ya wavu ya ‘African Championship’.
Mwishoni mwa wiki timu hiyo ililazimika kuvunja kambi yake waliyoiweka kwa zaidi ya wiki moja kutokana na kushindwa kumudu gharama za safari za kuelekea Morocco kwa ajili ya michuano ya hiyo ambayo baada ya Tanzania kujitoa sasa inajumuisha timu 23 za wanaume na 17 za wanawake.
Tanzania ilifanikiwa kufuzu hatua hiyo ya pili baada ya kufanikiwa kufanya vizuri katika mashindano ya awali yaliyofanyika katika fukwe za Lido zilizopo Entebbe, Uganda kuanzia Desemba 18 hadi 22, 2019.
Ushindi walioupata Tanzania dhidi ya Uganda, Kenya na Sudan uliwafanya kukaa juu ya msimamo wa kundi lao wakifuatiwa na Kenya ambao nao walifuzu kutinga hatua ya pili huku Sudan wakishika nafasi ya tatu na Uganda wakikaa nafasi ya mwisho.
Baada ya hapo walifanikiwa kupata uwenyeji wa mashindano hayo ambayo baadaye yaliahirishwa mara kadhaa kutokana na mlipuko wa Covid-19 uliozoikumba dunia na kusababisha shughuli mbalimbali ikiwemo michezo kusimamishwa.
Katibu Mkuu wa TAVA ambaye pia ni kocha wa timu ya Taifa ya wavu ufukweni, Alfred Selengia ameuambia Mtandao huu kuwa, baada ya kushindwa kupeleka timu Morocco, haraka sana wanahamishia mipango katika michuano ya ubingwa Afrika.
Amesema, kinachofanya kuanza haraka mipango kuelekea katika michuano hiyo itakayofanyika mwezi Sepemba ni funzo walizolipata baada ya safari yao ya Morocco kuota mbawa hivyo hawatarajii jambo hilo lije kujitokeza kwa mara nyingine.
“Hili la kuvuzu kwa michuano ya Olimpiki ilikuwa ghafla baada ya kuahirisha mara kadhaa kutokana na athari za Covid-19 hivyo sasa tupo kwenye harakati za kuanza haraka maandalizi na ‘African championship’ na tunachokisubiri sasa ni waandaaji wa mashindano ‘African Volleyball Confederation (CAVB) kutoa taarifa ya kuanza rasmi kwa mashindano hayo na yatafanyikia wapi,”.
Mbali na mashindano hayo ya Afrika, Selengia amesema pia wapo kwenye maandalizi ya michuano ya ndani ya klabu bingwa ya mwaka itakayoanza kutimua vumbi Julai 21 hadi 25 jijini Mbeya.
“Kwa sasa tumerudi pia kwenye kuendelea kutekeleza kalenda yetu ya mwaka ambapo Julai tutakuwa na michuano ya Taifa ya klabu bingwa itakayofanyika jijini Mbeya pamoja na chaguzi za vyama vya Mikoa,” amesema Selengia.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025