Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
BAADA ya kupata ushindi wa goli 3-2 dhidi ya Mwadui FC katika mchezo wa juzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliochezwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, vigogo wa klabu Yanga sasa wamefufua mikakati yao ili kuhakikisha timu hiyo inabeba ubingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup).
Katika mchezo huo, Mwadui walikuwa wa kwanza kupata goli lililofungwa dakika ya 7 na Anicent Revocatus ambalo lilisawazishwa dakika ya 22 na Bakari Mwamnyeto lakini dakika ya 65 Anicent aliifungia Mwadui goli la pili huku Yanga ikisawazisha dakika ya 90 kupitia kwa Yacouba Sogne huku Waziri Junior akifunga goli la ushindi lililowapa Yanga alama tatu na kufikisha alama 67 katika msimamo wa Ligi.
Licha ya kufikisha alama hizo 67 na kusalia na mechi tatu mkononi dhidi ya Simba, Ihefu na Dodoma Jiji FC ambapo wakishinda zote watakuwa na alama 76 bado Yanga wana nafasi ndogo ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu wa msimu huu kutokana na wapinzani wao Simba kubakiza alama sita ili kufikisha alama 76 ambazo zitawafanya kuwa mabingwa wapya wa msimu huu huku wakiwa na mechi nyingine mkononi.
Matumaini hayo hafifu ndiyo yanayowafanya vigogo wa Yanga kupanga kutangaza dau nono litakalowafanya wachezaji wao kupambana ili kupata ushindi katika mchezo wao wa nusu fainali dhidi ya Biashara United ambao watakuwa nyumbani katika dimba la Ally Hassan Mwinyi, Tabora.
Mmoja wa vigogo ambaye yupo kwenye kamati ya Mashindano ameambia Mtandao huu kuwa, wamejipanga kutangaza dau nono zaidi litakalowaongezea wachezaji morali ya kupambana na kufanya vizuri katika mchezo huo kwani hadi sasa matumaini yao makubwa yapo kwenye ubingwa huo.
“Licha ya kuwa bado tuna mechi za Ligi Kuu lakini matumaini ya kutwaa ubingwa wa msimu huu ni kidogo sana hivyo sasa mikakati yetu ipo kwenye michuano ya FA kwani tutahakikisha tunashinda nusu fainali na kisha fainali,” amesema kiongozi huyo.
Lakini kwa upande wake, Afisa Muhamasishaji wa klabu ya Yanga, Antonio Nugaz ameweka wazi kuwa, ushindi huo umefufu morali kubwa zaidi kuelekea katika mchezo wao wa nusu fainali ya FA dhidi ya Biashara ambao watahakikisha wanashinda ili kwenda fainali.
Amesema, tayari benchi lao la ufundi limeshaanza kuandaa mikakati imara itakayowawezesha kutwaa kombe hilo ili kurudi katika mashindano ya kimataifa lakini pia kuwapa furaha mashabiki wao ambao wamekuwa wakiwaonesha sapoti kubwa.
Kocha wa makipa wa Yanga, Razack Siwa amesema, baada ya kushinda mchezo huo sasa wanarudi kurekebisha makosa waliyoyaona ili kuhakikisha wanakuwa bora zaidi katika mchezo huo wa FA dhidi ya Biashara.
Amesema kuwa, ukiangalia katika mchezo huo wachezaji wao walifanya makosa kadhaa hasa katika safu ya ulinzi na ushambuliaji ambayo yalisababisha wapinzani wao kuanza kufunga na kisha wao kuja nyuma na kusawazisha lakini Mungu akawasaidia wakapata ushindi.
“Siku zote mpira ni mchezo wa kutumia nafasi lakini sisi tulitengeneza nafasi nyingi ambazo baadaye tulishindwa kuzitumia jambo lililosababisha kupata ushindi dakika za mwishoni hivyo kuna vingi vya kwenda kubadili katika siku zilizobaki ili kushinda mchezo ulio mbele yetu,” amesema Siwa.
Katika hatua nyingine, wakati Yanga wakianza maandalizi ya mchezo huo, Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Dkt. Mshindo Msolla kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji wameweka hadharani ajenda zitakazojadiliwa katika mkutano mkuu utakaofanyika Juni 27 katika ukumbu wa DYCCC, Chang’ombe.
Katika Mkutano huo utakaofanyika kwa mujibu wa katiba ya Yanga, moja ya mambo makubwa yatakayojadiliwa ni kupokea na judili taarifa za kazi kutoka kwa Kamati ya Utendaji, kuthibitisha hesabu za fedha zilizokaguliwa kwa mwaka uliotangulia na kuthibitisha taarifa za chombo cha ukaguzi nah atua zilizochukuliwa na vyombo vya utendaji.
Pia watathibitisha bajeti yam waka ujao, uchaguzi wa nafasi zilizo wazi, kupitia mapendekezo ya marekebisho ya Katiba na taratibu za Yanga pamoja na majadiliano ya mapendekezo yaliyowasilishwa na wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025