Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
WAKATI kikosi cha timu ya Coastal Union leo wakitamba kuchukua alama zote tatu katika mchezo wao wa nyumbani wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaochezwa kwenye uwanja wa Nelson Mandela, wapinzani wao Coastal Union wameapa kuwamaliza kwao.
Timu hizo zinakutana huku kila mmoja akihitaji ushindi baada ya kupoteza mechi zao zilizopita ugenini baada ya Prisons kuchapwa goli 1-0 na Kagera Sugar huku Coastal akidondosha alama zote tatu kufuatia kichapo cha goli 2-0 katika mchezo dhidi ya Mbeya City.
Mbali na jambo hilo, makocha wa timu zote mbili wameapa kuutumia mchezo huo kuoneshana ubabe baada ya Desemba 13 kugawana alama moja katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliomalizika kwa suluhu.
Kocha msaidizi wa Prisons, Shaban Kazumba amesema kuwa, wanahitaji sana alama tatu katika mchezo huo ambao pia utawapa morali kuelekea kwenye mechi zao mbili zitakazosalia ambazo walishindwa kutamba baada ya kutoka 1-1 na Gwambina na kukubali kichapo cha goli 2-0 kutoka kwa Biashara United.
Amesema, kile walichoshindwa kukifanya katika mechi yao ya kwanza katika uwanja wa Mkwakwani wanakwenda kukakamilisha katika mchezo wao wa leo na wapinzani wao wasitarajie kuambulia hata alama moja.
Kocha huyo amesema kuwa, maandalizi waliyoyafanya hadi sasa yanawapa uhakika wa kubakiza alama zote tatu nyumbani ambazo zitawaweka kwenye nafasi nzuri zaidi katika msimamo wa Ligi Kuu msimu huu.
“Baada ya kupoteza mchezo wetu kwa Kagera tulihamishia nguvu katika mechi zetu tatu za nyumbani zilizosalia msimu huu tukianza nay a leo dhidi ya Coastal Union ambazo tunatakiwa kushinda ili kujiweka kwenye nafasi nzuri zaidi katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzanania,” amesema Kazumba.
Licha ya tambo hizo za Kazumba, kocha mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda alisema ana uhakika mbinu watakazoingia nazo leo zitawabeba na kuwapa alama tatu zitakazowaondosha kwenye hatari ya kushuka daraja kwani nafasi waliyokaa kwenye msimamo wa Ligi ni mbaya.
Amesema, kutokana na jambo hilo, watahakikisha wanaingia katika mchezo huo kucheza kufa na kupona ili kupata wanachokihitaji na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kusalia kwenye Ligi msimu ujao.
“Tupo kwenye nafasi mbaya na tunahitaji kujikwamua ili kusalia kwenye Ligi msimu ujao hivyo ni lazima leo tucheze kwa jihadi kwani kwa sasa alama tatu ni muhimu zaidi kuliko kitu chochote kwa sasa,” amesema Mgunda.
More Stories
Watumishi wa Fahari wafanya Bonanza
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship