Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam.
SHIRIKA la Legal Services Facility (LSF) limezindua mfumo wa kitumizi cha simu za mkononi unaojulikana kama HAKI YANGU App, ambao, unaweza kumsaidia mwananchi kupata msaada wa kisheria popote alipo kupitia simu yake ya mkononi.
Uzinduzi wa mfumo huo umefanyika jijiji Dar es Salaam ambapo umebuniwa na LSF na umewaunganisha wasaidizi wa kisheria takribani 4,000 nchi nzima na kupitia mfumo huo wanaweza kukutanishwa na mwananchi mwenye uhitaji wa huduma za msaada wa kisheria ama wasaidizi wa kisheria na kuweza kusaidiwa.
Mfumo huo ni wa kwanza kubuniwa na wa aina yake nchini Tanzania, ambao utamsaidia mwananchi kuwasiliana moja kwa moja na msaidizi wa kisheria au mtoa huduma za msaada wa kisheria kupitia simu ya mkononi kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno au kupiga simu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo huo jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala amesema kuwa, LSF imebuni mfumo wa HAKI YANGU App ili kuendelea kuhakikisha kuwa, huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria nchini Tanzania zinapatikana kiurahisi zaidi kwa kuwa, upatikanaji wa huduma hiyo imekuwa ni changamoto katika jamii licha ya umuhimu wake.
“Kwa uzoefu wa LSF katika kutekeleza mradi wa upatikanaji wa haki nchini tumeona kuwa, wananchi walio wengi bado wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto hivyo njia hii itachochea upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa urahisi zaidi mahali popote kupitia simu ya mkononi,” amesema Ng’wanakilala na kuongeza;
“Kwa miaka 10 sasa, sisi kama LSF tumekuwa tukiwezesha mashirika yanayotoa huduma za msaada na wasaidizi wa kisheria zaidi ya 200 nchi nzima ili kutoa huduma hiyo muhimu katika jamii bure. HAKI YANGU App ni muendelezo tu wa utekelezaji wa mradi wetu unaolenga kuwa na jamii iliyowezeshwa kisheria kwa kutoa huduma za msaada wa kisheria bure kwa wananchi wote,”amesema Mtendaji Mkuu wa LSF.
Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema LSF imekuwa ni mdau muhimu wa Serikali hasa katika sekta ya msaada wa kisheria kwa kuwa imekuwa mstari wa mbele kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wananchi kupitia mradi wake wa upatikanaji wa haki.
“LSF imekuwa ikichagiza mabadiliko ya kisera na kimfumo katika sekta ya msaada wa kisheria kwa kushirikiana kwa karibu sana na Serikali.
“Mwaka 2017 tulishirikiana kwa karibu katika kuhakikisha sheria ya msaada wa kisheria inatungwa ili kuwezesha wananchi wetu kupata haki zao kupitia huduma za msaada na wasaidizi wa kisheria,” amesema Profesa Kabudi.
Profesa Kabudi amesema, amefurahi kuona LSF wamekuja na mfumo ambao utasogeza huduma karibu zaidi kwa wananchi wanaohitaji huduma ya msaada na wasaidizi wa kisheria.
Ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inatambua mchango walionao wadau wa maendeleo nchini Tanzania ikiwemo sekta binafsi pamoja sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali katika kuunga juhudi za Serikali kwenye kuboresha huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo huduma ya msaada wa kisheria na upatikanaji wa haki kwa ujumla kwani ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya kijamii na uchumi kwa ujumla.
“Serikali sasa iko katika kutekeleza mchakato wa kutafisiri sheria kwa lugha ya Kiswahili. Hii ni moja ya hatua muhimu katika kuhakikisha tunawawezesha wananchi kuelewa sheria na kudai haki zao pale zinapopotea.
“Naipongeza sana LSF kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika suala hili la kutafsiri sheria kwa lugha ya Kiswahili na kwa kuendelea kutekeleza mradi wake mkubwa nchini Tanzania, ambao kwa kiasi kikubwa umeweza kusaidia maelfu ya wananchi walio kwenye mazingira magumu hususani wanawake na watoto kupata haki zao kutokana na kazi nzuri inayofanywa na wasaidizi wa kisheria nchi nzima,”amesema Profesa Kabudi.
Amefafanua kwamba, kupitia mfumo huu wananchi wengi wakiwemo kina mama na watoto wataweza kupata msaada wa haraka zaidi pale wanapokutana na changamoto mbalimbali zinazohusiana na kuminywa ama kukandamizwa kwa haki zao kutokana na sababu mbalimbali kama vile jinsia au umri wao,” alisema Profesa Kabudi.
Faida za mfumo
Mfumo huo unaweza kumsaidia mwananchi kuongeza uelewa wa masuala mbalimbali ya kisheria kwa kujifunza kupitia taarifa za jumla za masuala ya kisheria zilizowekwa katika mfumo huo kwa lengo la kuelimisha jamii juu ya masuala yanayohitaji utatuzi wa kisheria kupitia mifumo rasmi na isiyo rasmi ya utoaji haki kama vile huduma za msaada na wasaidizi wa kisheria.
Mfumo huu utawezesha wasaidizi wa kisheria kupata mafunzo ya kozi mbalimbali kimtandao na kuendelea kuboresha uwezo wao ili kutoa huduma bora na yenye ufanisi zaidi.
Kuhusu LSF
LSF ni shirika linalofadhiliwa na wadau wa maendeleo, ambao ni Umoja wa Nchi za Ulaya nchini Tanzania na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Denmark (DANIDA) kupitia ubalozi wa Denmark katika kutekeleza mradi wa upatikanaji wa haki nchini Tanzania.
Chini ya ufadhili huu, LSF inatekeleza mradi wa upatikanaji wa haki katika kila mikoa na wilaya Tanzania bara na Zanzibar, ambapo takribani watu millioni 6 wanafikiwa kwa kupatiwa elimu juu ya masuala ya kisheria, na kesi takribani 90,000 zimewafikia watoa huduma za msaada wa kisheria, ambapo asilimia 60 za mashauri hayo yameweza kutatuliwa na watoa huduma hao (Ripoti ya LSF 2020).
More Stories
Tanga kutumia vituo 5405,kupiga kura leo
NMB yatoa msaada wa vifaa Mufindi
Viongozi wa dini Katavi waomba wananchi kujitokeza kupiga kura