Na Bakari Lulela,Timesmajira Online.
WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, wamefanya ziara katika Ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), ili kujionea jinsi taasisi hiyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu inavyosimamia uzingatiaji wa viwango vya usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini.
Ziara hiyo imetokana na taarifa ya utekelezaji majukumu ya OSHA kwa mwaka 2020/21, iliyowasilishwa kwenye kamati hiyo Machi mwaka huu ambapo kamati iliridhishwa na utendaji na hivyo, kuagiza kuandaliwa kwa ziara kwa ajili ya kamati kuona uhalisia wa masuala ambayo wamekuwa wakiwasilishiwa kupitia taarifa mbalimbali.
Akizungumza baada ya kutembelea ofisi za OSHA, Kiwanda cha Sigara (TCC) na Kiwanda cha Gypsum cha Knauf (Knauf Gypsum Tanzania Limited) kilichopo Mkuranga, ambako walikwenda kuangalia jinsi viwanda hivyo vinavyotekeleza miongozo inayotolewa na OSHA Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Najma Gigi amesema wameridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na OSHA katika kutoa miongozo ya kulinda nguvu kazi kwenye maeneo ya kazi hapa nchini.
“Ziara yetu imefana na suala tulilolifuatilia la usalama na afya mahali pa kazi kwa kweli hapa, tumeona linazingatiwa ipasavyo jambo ambalo linafanya kampuni hii kufanya vizuri katika uzalishaji. Hivyo tumefurahi sana na tunaamini kwamba mtaendelea kufanya vizuri,” amesema Najma.
Nao baadhi ya Wajumbe wa Kamati hiyo wakiwa wameambatana na Mwenyekiti wao wamesema kupitia ziara hiyo, wameweza kutambua kazi kubwa inayofanywa na OSHA katika kuhakikisha kwamba mazingira ya kazi yanakuwa salama.
“Nitumie fursa hii kuipongeza Menejimenti ya OSHA pamoja na Waziri, Jenista Mhagama kwa kazi kubwa wanayofanya kiukweli wakati mwingine unaweza usione umuhimu wa taasisi hizi kama usipofika katika maeneo wanayosimamia, sisi hapa tumejionea wenyewe kazi kubwa inayofanywa na OSHA katika kutoa miongozo na ushauri wa namna ya kuboresha mazingira ya kazi, sisi kama Wabunge tuna kazi kubwa ya kuunga mkono kazi hii na kuishauri serikali kuiongezea OSHA bajeti ili iweze kupanua wigo wa shughuli hizo za ukaguzi katika maeneo ya kazi,” amesema Elibariki Kingu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki na Mjumbe wa kamati.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amesema serikali imekuwa ikitegemea ushauri wa Kamati za Bunge, ili kuweza kutekeleza mipango yake ipasavyo.
“Sisi kama serikali, tunaweza tukawa tumejifungia ndani na kutengeneza mipango mbalimbali ya maendeleo lakini ili mipango hiyo iweze kutekelezeka na kuwa na tija kwa wananchi, tunategemea sana ushauri kutoka kwa Wabunge hususan Kamati ya Katiba na Sheria ambao ndiyo wawakilishi wa wananchi,” amesema.
Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema kupitia ziara hiyo Wajumbe walipata fursa ya kujionea hali halisi ya usalama na afya katika maeneo ya kazi hapa nchini.
“Kpitia ziara hii Waheshimiwa Wabunge, wamejionea jinsi ambavyo OSHA imejipanga kulinda nguvu kazi ya nchi na kwa kweli wamefarijika sana ma wamekiri kwamba yale ambayo wamekuwa wakiyaona katika taarifa zetu, ndiyo ambayo tunayatekeleza kwenye sehemu za kazi na hivyo kufanya wawekezaji kupata tija katika uzalishaji,” amesema.
More Stories
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi
Mbunge Ndingo:CCM imejidhatiti kuwaletea maendeleo wananchi
SACP Katabazi: Elimu ya usafirishaji wa kemikali bado ni muhimu kwa watanzania