Na Adili Mhina,TimesMajira online,Mtwara
NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu,Gerald Mweli ametoa onyo kwa watumishi wa Halmashauri zote nchini wanaosuasua kuingiza kwenye mfumo walimu waliopanda madaraja ikiwa ni sehemu ya kukamilisha taratibu za kiutumishi.
Ametoa kauli jana Juni mjini Mtwara wakati wa kikao chake kilichowahusisha Maafisa Elimu wa Mikoa,Maafisa Taaluma pamoja na Maafisa Elimu wa Wilaya wa Shule za Msingi ambao wapo mkoani hapo kwa lengo la kushiriki michenzo ya kitaifa ya wanafunzi wa shule za msingi (UMITASHUMTA) na sekondari (UMISSETA).
Amesisitiza kuwa kila mwalimu aliyepandishwa daraja ni lazima aingizwe kwenye mfumo kabla ya Juni 12 ambayo ndiyo siku ya mwisho ya kufanya zoezi hilo kwa mujibu wa maelekezo kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
“Tumeshatoa maelekezo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote kwamba zoezi la kuingiza watumishi kwenye mfumo linatakiwa limalizike Juni 12. Sasa ninashindwa kuelewa kwa nini baadhi ya watumishi wanaohusika bado wanajivuta katika kukamilisha zoezi hili,” amehoji.
Ameongeza kuwa ni wajibu wa Afisa Elimu katika kila Halmashauri kuhakikisha anafanya kazi kwa karibu na Maafisa Utumishi ili kuhakikisha walimu waliopandishwa madaraja wanaingizwa kwenye mfumo ndani ya muda uliopangwa huku akiwataka Maafisa Elimu ambao Halmashauri zao hazijaanza zoezi hilo kurudi kwenye maeneo yao ya kazi mara moja kushughulikia zoezi hilo.
“Najua tumekuja hapa kwa ajili ya michezo, lakini hakuna sababu ya Afisa Elimu kuendelea kukaa hapa wakati huko kwake zoezi la kuingiza walimu kwenye mfumo halifanyiki na siku zimebaki chache. Hivyo, ninasema wale wote wanaojua kuwa hawajaanza kutekeleza zoezi hilo kesho (leo) warudi kwenye vituo vyao vya kazi na kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kama ilivyoelekezwa” amesisitiza.
Ameendelea kueleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliamua kumaliza kero ya watumishi wa Umma wakiwemo walimu kuhusu kutopanda madaraja kwa muda mrefu na kutoa maelekezo kuwa watumishi wenye sifa wapandishwe, hivyo ofisi yake haiko tayari kuona mtumishi yeyote anakwamisha zoezi hilo.
“Siku chache tu zilizopita ilikuwa kila ninapokutana na walimu kilio chao kikubwa kilikuwa ni suala la kupanda madaraja, leo Mheshimiwa Rais ametoa kibali tuwapandishe halafu tunaanza kujivuta tena. Ninasisitiza mtumishi yeyote anayejaribu kukwamisha zoezi tutashughulika naye bila kuchelewa,” mweli amesisitiza.
Awali, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paulina Nkwama alisema kuwa ofisi yake inafuatilia kwa karibu zoezi la kuingiza walimu kwenye mfumo na imejiwekea utaratibu wa kupata taarifa ya idadi ya walimu wanaoingizwa kwenye mfumo kutoka Halmashauri zote kila siku.
Amesema pamoja na kwamba Halmashauri nyingi zinaendelea kutekeleza zoezi hilo, zipo baadhi ya Halmasahuri ambazo utendaji wao hauridhishi jambo ambalo lisipofanyiwa kazi kwa wakati linaweza kuathiri kukamilika kwa kazi hiyo kwa wakati.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi