November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wahamasishwa kutumia gesi kuhifadhia mbegu za upandikizaji

Na Hadija Bagasha , TimesMajira Online, Tanga

MTAALAMU wa gesi na mimea mkoani Tanga amewashauri wakulima na wafugaji nchini kutumia gesi ili kuhifadhia mbegu kwa ajili ya upandikizaji wa majike, lakini pia kwa wafugaji wa samaki nao wanatakiwa watumie gesi aina ya oxygen ndani ya maji ili kuwakuza samaki kwa haraka na hatimaye kuongeza uzalishaji kwenye sekta hizo.

Omar Abanoor kutoka kiwanda cha Oxygen Products East Africa Company Ltd ( OPEL) alitoa ushauri huo hivi karibuni wakati wa maonesho ya wadau wa maziwa Nchini yaliyofanyika katika viwanja vya Tangamano jijini humo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya unywaji wa maziwa Duniani ambayo ilianza mei 31.

Abanoor amesema, sekta hizo mbili za kilimo na ufugaji zinatakiwa kutumia gesi ili kuongeza ufanisi na uzalishaji kwani matumizi ya mbegu bora yanaweza kuwasaidia kuwa na mifugo bora itakayoweza kuingia kwenye soko la ndani na nje ya nchi.

“Mfugaji anatakiwa atumie gesi aina ya Nitrogen kwa ajili ya kuhifadhia mbegu kwa ajili ya upandikizaji wa majike, lakini pia kwa wafugaji wa samaki nao wanatakiwa watumie gesi aina ya oxygen ndani ya maji ili kuwakuza samaki kwa haraka sana, lakini pia wanakuwa na afya nzuri na uhakika wa soko sehemu yoyote Duniani,”amesema.

Amesema, matumizi ya gesi kwa wafugaji pia ni kwenye usafi wa maeneo ya kuhifadhia maziwa kwa ajili ya kuua bakteria na wadudu wengine.

“Wafugaji wanatakiwa wahifadhi maziwa yao kwakupulizia gesi hii kwaajili yakuua wadudu na kuhifadhi kwa muda mrefu bila kuharibika pamoja na kuondoa harufu mbaya , kwakufanya hivyo hawatoweza kupata hasara,”amesema Abanoor.

Amesema, kwa upande wa wakulima wao wanahitaji matumizi ya gesi kwa kuwa yanawasaidia kuongeza afya ya mimea ambayo ndio chakula kikuu cha wanyama.

“Wakulima lazima watumie mbegu bora kwa ajili ya malisho, hivyo gesi husaidia kuongeza ubora wa mbegu na kutunza mimea kuwa na afya bora muda wote,”amesisitiza.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema,wafugaji nchini wanakabiliwa na matatizo mengi ya uzalishaji ikiwemo malisho duni hali inayosababisha kukosa soko la maziwa.

“Malisho duni na ukosefu wa Elimu na Teknolojia ni kikwazo, hatuwezi kuzuia maziwa ya nje, lakini ni lazima tushindane kwa ubora wa bidhaa, Serikali itaendelea kuwasaidia wafugaji na wasindikaji nchini ili kuondoa matatizo yao,”amesema.

Amesema, kwa sasa wafugaji wanazalisha zaidi lita bilioni tatu huku robo tatu yake ikiwa ni kutoka ng’ombe wa asili.

“Ng’ombe wa asili bado ni tegemeo kubwa sana ndani ya nchi yetu, hivyo matumizi ya teknolojia yaongezeke ili kuwasaidia wafugaji kuongeza uzarishaji nchini,”amesisitiza Prof. Gabriel.