November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

KITS yatekeleza agizo la Rais Samia kuhamasisha uwekezaji nchini

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KAMPUNI ya Kimataifa inayojihusisha na masuala ya Utalii ya Kilimanjaro International Tourism and Safaris (KITS), imekuwa balozi mzuri na lango la kuingiza watalii na wawekezaji nchini kutoka majimbo 50 ya nchini Marekani ambapo kwa sasa wameleta wawekezaji wakubwa wawili kutoka Marekani ili kuhamasisha uwekezaji nchini.

Akizungumzia kuhusu hilo, leo mkoani Dar es Salaam,Mkurugenzi Mtendaji (CEO) wa KITS, Vonnie Kiondo, amesema hatua hiyo imefikiwa ili kutekeleza azma ya Serikali ya kuongeza mahusiano ya Kimataifa, uwekezaji na Utalii hivyo wameleta wafanyabiashara wakubwa wawili kutoka Marekani kwa ajili ya kuitembelea Tanzania.

Vonnie ambaye ni mmiliki wa Kampuni hiyo, yenye Makao Makuu yake Washington DC, Marekani huku kwa upande wa Tanzania ina ofisi zake Njiro, Arusha, amewataja wafanyabiashara hao wakubwa ambao KITS imeratibu safari zao kuwa ni CEO wa Kampuni ya Affinity Travel Group na bilionea Miguel Pilgram ambaye ni CEO wa The Pilgram Group.

Wageni hawa waliofika Juni 3 mwaka huu wanatarajia kuondoka nchini Juni 11, mwaka huu baada ya kufanya mikutano ya uwekezaji katika sekta ya utalii kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Wizara ya Mambo ya Nje naushirikiano wa Afrika Mashariki na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Amesema katika ziara ya wageni hao watakutana na wasanii mbalimbali wa Tanzania katika kuona namna ambavyo wasanii wanaweza kufanya sanaa zao, ikiwemo na kutembelea jiji la Dar es Salaam, Wilaya ya Bagamoyo na Zanzibar.

“Tunatarajia ziara hiyo kuwa na faida kubwa na miongoni ni kuuza na kutangaza wasanii na wanamuziki wetu nchini.” Amesema na kuongeza kuwa, “Tunatarajia ziara hiyo iweze kuongeza ajira miongoni mwa Watanzania, kuongezeka kwa mapato ya kiuchumi katika sekta mbalimbali zinazohusiana na Utalii na ukarimu ukiwa ni pamoja na kuuzwa nje kwa bidhaa na mavazi ya asili.”