November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yanga: Sio FA tu, ubingwa VPL wetu

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KUTOKANA na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufika katika fainali za msimu huu za michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam ‘Azam Sports Federation Cup’, Uongozi wa Yanga umesema mkakati wao haupo tu kwenye kubeba taji hilo bali hata lile la Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL).

Juzi Yanga iliibuka na ushindi wa goli 2-0 dhidi ya wenyeji wao Mwadui FC katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga hivyo sasa watakutana na Biashara United ambao watakuwa nyumbani katika mchezo wa nusu fainali utakaochezwa mwezi ujao katika uwanja wa Ally Hassan Mwinyi.

Kitendo cha Yanga kufika katika hatua hiyo kinawaaminisha kuwa wataweza kufanya vizuri na kwenda fainali hasa kutokana na rekodi bora waliyonayo dhidi ya Biashara ambao walikubali vichapo katia mechi zote mbili za msimu huu ukilinganisha na misimu miwili ya nyuma.

Licha ya kuamini hivyo lakini huenda wakakutana na kipingamizi kutoka kwa wapinzani wao ambao wameapa kufanya maajabu katika michuano hiyo kutokana na kiu yao kubwa ya kutaka kuiwakilisha nchi kimataifa.

Mara baada ya jana kikosi cha Yaga kuwasili Dar es Salaam wakitokea Shinyanga, Benchi la ufundi limeweka wazi kuwa hawatakuwa na muda wa kupoteza na haraka sana wataanza maandalizi kwa ajili ya mechi zao tano zilizosalia za Ligi Kuu.

Katika mechi hizo, Yanga itakuwa mgeni wa Maafande wa Ruvu Shooting katika machezo wa Juni 17 lakini Juni 20 watakuwa nyumbani kuvaana na Mwadui FC ambao tayari wameshashuka daraja.

Julai 3, watacheza mchezo wao wa kiporo dhidi ya Watani wao wa Jadi Simba, watawakaribisha Ihefu Julai 14 na kisha watawafuata Dodoma Jiji FC katika mchezo wa mwisho wa Ligi utakaochezwa kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Ikiwa Yanga itafanikiwa kuvuna alama zote 15 katika mechi hizo tano basi watafanikiwa kufikisha pointi 76 lakini wakiwaombea dua mbaya Simba ambao hadi sasa wamekaa kileleni mwa msimamo wa Ligi wakiwa na alama 61 huku wakiwa na mechi tisa mkononi.

Kama Simba watafanikiwa kushinda mechi tano tu kati ya hizo tisa kwa wastani mzuri wa mabao basi watazima ndoto za Yanga za kutwaa taji hilo msimuu na kuwapa kazi kubwa ya kujipanga kwa ajili ya msimu ujao ambao bingwa ataondoka na bonasi ya Sh. milioni 500 kutoka kwa Azam Media ambao wametangaza udhamini wa Sh. bilioni 225.6 wa haki ya matangazo ya televisheni kwenye mechi za Ligi hiyo.

Akizungumza na Mtandao huu, kocha wa makipa wa Yanga, Razack Siwa amesema, licha ya kuwepo kwa tofauti ya michezo baina ya timu zinazowania ubingwa msimu huu lakini wanaamini bado wapo kwenye nafasi nzuri ya kutwaa taji la Ligi ikiwa watatumia vema mechi zao.

Kama wapambanaji hawawezi kukata tamaa na ndio maana wanarudi kambini haraka ili kuanza kujipanga kwa ajili ya mechi hizo muhimu kwani kwa sasa kazi kubwa iliyo mbele yao ni kurekebisha makosa yaliyojokeza katika mchezo wao uliopita.

Amesema kuwa, eneo ambalo watalishughulikia zaidi ni safu yao ya ushambuliaji ambayo imeshindwa kutumia vema nafasi wanazotengeneza kwani hata uliangalia katika mchezo wao uliopita walipiga mashuti 19, tisa yakilenga lango lakini waliambulia goli 2.

“Baada ya kumaliza kazi katika michuano ya FA na kuinusa fainali sasa tunarudisha nguvu katika mechi zetu zilizosalia za Ligi Kuu ambazo tunaamini tukizitumia vema basi ubingwa utatua klabuni kwetu,”.

“Tutahakikisha tunatumia mapumziko wa Ligi kusimama kupisha kalenda ya FIFA kati ya Mei 31 hadi Juni 15 kurekebisha makosa yetu lakini pia kukiongezea makali kikosi ili kubeba alama tatu katika kila mchezo na kupata tunachokihitaji,” amesema kocha huyo.