Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
BONDIA wa Kimataifa wa Tanzania, Hassan Mwakinyo ameahidi kumpa kichapo kikali mpinzani wake Antonio Mayala kutoka Angola ikiwa kama asante kwa Rais wa kwanza mwanamke hapa nchini Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan.
Mwakinyo atambanda ulingoni kesho kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Masaki katika pambano la kuwania mkanda wa Afrika (ABU) uzito wa ‘Super Welter’ lililoandaliwa na Kampuni ya Jackson Group Sports.
Amesema kuwa, amejiandaa vyema na kwa vile atakuwa anapigana kwa mara ya kwanza chini ya uongozi wa Rais Samia, hatofanya makosa zaidi ya kushinda tena raundi za mwanzoni tu katika pambano hilo lililodhaminiwa na KCB Bank, Plus TV, Multichoice Tanzania, Tanzania Tourism Board, Onomo Hotel, Precision Air, Prestine Logistics, Urban Soul na washirika wa kimataifa Global Boxing Stars na Epic Sports Entertainment.
“Nitakuwa napigana kwa mara ya kwanza chini ya Rais Mama Samia Suluhu Hassan. Sitamuwangusha Rais na watanzania kwa ujumla, nawaomba mashabiki kufika kwa wingi ili kunipa sapoti,” amesema Mwakinyo.
Wakati Mwakinyo anasema hayo, mpinzani wake Mayala amesema kuwa, pamoja na kupata taarifa za muda mfupi, amejiandaa vyema ili kuonyesha kuwa yeye ni bondia bora wa ngumi za kulipwa.
“Nimekuja kwa ajili ya kushinda na si kupoteza, nilikuwa nafanya mazoezi kwa sababu ngumi ni kazi yangu na siwezi kuruhusu Mwakinyo kushinda na kuchukua mkanda wa Afrika hata kama yupo katika ardhi yao ya nyumbani,” amesema Mayala.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Jackson Group Sports, Kelvin Twissa amesema, mbali ya pambano hilo, bondia Daniel Matefu atazichapa na bondia kutoka Bulgaria, Pencho Tsvetkov huku bondia wa kike Leila Yazidu atazichapa na bondia wa Bulgarian Joana Nwamerue.
Hamisi Palasungulu atazichapa na bondia wa Congo Brazzaville, Ardi Ndembo huku Imani Daudi Kawaya akionyeshana kazi na bondia kutoka Afrika Kusini Chris Thompson.
Katika pambano lingine la ABU, bondia Shabani Jongo chini ya Mnigeria Olanrewaju Durodora ambao watawania uzito wa juu na nyota mwingine Ibrahim Class atazipiga na bondia wa Afrika Kusini, Sibusiso Zingange.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025