Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
KOCHA mkuu wa kikosi cha timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’, Bakari Shime ‘Mchawi Mweusi’ ameendelea kukinoa kikosi chake huku akiwagomea timu ya Taifa ya Malawi kucheza nao mchezo wa kirafiki kuelekea katika mchezo wao wa mzunguko wa kwanza wa kuwania kufuzu kucheza Kombe la Mataifa Afrika kwa wanawake ‘Women Africa Cup of Nation (AFCON)’.
Katika michuano hiyo ya kimataifa, Twiga Stars itavaana na timu ya Taifa ya Namibia huku wagodo zao timu ya Taifa ya wasichana wenye umri chini ya miaka 20 wenyewe watatupa karata yao dhidi na mshindi wa mechi kati ya Djibouti na Eritrea katika mzunguko wa pili wa kufuzu Kombe la Dunia ‘African Qualifiers FIFA U 20 Womens World Cup Costa Rica 2022’.
Kwa upande wa timu ya Taifa ya Tanzania ya wasichana wenye umri wa miaka 17, wenyewe wamepangiwa kuanza na Botswana katika mchezo wa raundi ya kwanza wa kusaka tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia kwa wasichana wenye umri huyo (U-17 FIFA Women’s World Cup Qualifier 2022 India) katika mchezo utakaochezwa kati ya Januari 13-29.
Shime ameumbia Mtandao huu kuwa, kuelekea katika mashindano hayo wanahitaji sana mechi za kirafiki za kimataifa ambazo wanaendelea kufanya utaratibu wa kusaka timu ambayo itakuwa kipomo sahihi kwao.
Amesema, wakiwa wanasaka mechi hizo timu ya Malawi imeomba kucheza nao mechi ya kirafiki lakini hawatocheza nao kwani huenda wakaja kukutaka na timu hiyo katika raundi zinazofanya jambo ambalo huenda likawaathiri.
Akizungumzia maendeleo ya kambi yao, kocha huyo amesema kuwa, kadri siku zinavyokwenda ndivyo wachezaji wake wanavyozidi kuimarika na ana matumaini makubwa na wachezaji wake ambao wameonesha viwango bora na kufanya vizuri katika michuano ya Ligi ya Kuu Wanawake maarufu kama Serengeti Lite Premium League iliyomalizika hivi karibuni kwa Simba Queens kutwaa ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo.
“Tunahitaji sana mechi za kirafiki kwa ajili ya kupima kikosi chetu na unahitaji kupata timu itakayotupa ushindani sahihi ili kuweza kubaini maeneo ambayo tunatakiwa kuyafanyika kazi zaidi kabla ya mchezo wetu wa kwanza,”.
“Kwa sasa kazi kubwa iliyo mbele yetu ni kupata timu hiyo pamoja na kuhakikisha tunawapa mbinu bora ambazo zitaimarisha zaidi viwango vyao na kuweza kupata matokeo bora yatakayotuwezesha kufika mbali kwani tunakwenda kukutana na timu tunayotoka nayo ukanda tofauti wa kisoka hivyo ni lazima tufanye maandalizi bora zaidi na kufanyia kazi mbinu zao kwani mkakati wetu ni kufanya vizuri na nina uhakika itakuwa hivyo,” amesema Shime.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025