November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB yawapatia mafunzo waendesha Pikipiki

Na Mwandishi Wetu,TimesMajiar Online Dodoma

ZAIDI ya vijana 200 wanaojishughulisha na usafirishaji wa abiria kwa kutumia Pikipiki bodaboda na Bajaji, mwishoni mwa juma walipatiwa mafunzo ya namna ya kujiongezea kipato yaliyotolewa na benki ya NMB.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwapa elimu ya mikopo inayotolewa na benki hiyo katika mpango wao wa miliki chombo na NMB ambao umetenga Sh. bilioni 5 katika kundi hilo.

Wengi wa vijana hao ni wahitimu wa vyuo vikuu ambao waliamua kujiajiri kupitia Pikipiki hizo, hata hivyo wameiomba NMB kuangalia upya sharti la mtu kuwekeza asilimia 20 ndipo akopeshwe kwamba litazamwe kwani inawakosesha fursa vijana wengi.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa mikopo ya Pikipiki hizo, Mwendesha boda boda jijini Dodoma Chacha Marwa amesema, mpango wa NMB ni mkombozi kwa vijana ambao wanaanza maisha kwa kuwa utasaidia kuwapatia vifaa vya kuwaingizia kipato.

Marwa ambaye ni mhitimu wa Shahada ya sayansi ya baiolojia ya Chuo Kikuu cha Dodoma, amesema mpango wa kusubiri ajira unawachelewesha na kuwapotezea malengo vijana wengi lakini kwenye bodaboda na Bajaji kuna fedha zaidi ya mshahara.

“Binafsi nimepita katika mapito mengi, nimeendesha bodaboda za watu nikaingia mikataba lakini hadi sasa naendesha gari ndogo yangu na pikipiki nimewapa vijana,” ili waniletee kipato,” amesema Marwa.

Akizungumzia asilimia 20 ambazo zinatakiwa na NMB kama zamana ya kiasi hicho, kinawakosesha sifa vijana wengi licha ya kuwa wanauwezo wa kurejesha lakini ni pale wanapoanza maisha huwa hawana kianzio.

Chacha amesema, kama benki ingetengeneza utaratibu wa kuwapatia vijana bila kuweka hiyo asilimia ingekuwa mkombozi mkubwa kwa vijana wengi ambao huzunguka na vyeti kusaka ajira bila mafanikio.

Naye Meneja wa NMB kanda ya kati Nsolo Mlozi amesema, miliki chombo na NMB imeshafika katika mikoa ya Dar es Salaam,Mwanza na Dodoma huku sehemu kubwa ikilenga vijana wanaoanza maisha.

Mlozi amesema, benki hiyo hutumia changamoto zinazojitokeza kwa Watanzania na kuwapelekea mawazo kuwa fursa, hivyo mambo mengi wanayozungumza vijana yanafanyiwa kazi kwa kufuata taratibu.

Kwa upande wake Naibu Meya wa Jiji la Dodoma Emmanuel Chibago ameiomba benki kuwawezesha vijana hao kupitia Umoja wa Mabajaji na Pikipiki Dodoma (UMAPIDO) kwani wamekuwa wasimamizi wazuri kwa wanaokopa.

Chibago ametolea mfano kuwa mwaka jana halmashauri ya Jiji la Dodoma ilitoa mkopo kwa UMAPIDO wa Sh305 milioni lakini hawajawahi kuchelewesha marejesho na kila mwezi wanarejesha Sh12.5 milioni.

Kwa upande wake Naibu Meya amewataka vijana kuwa waaminifu kwa Taasisi na mashirika yanayowatambua na kuwapatia mikopo ili waweke malengo ya kujikomboa kimaisha.

%%%%%%%%%%%%%