Na Nuru Mkupa, Dodoma
ASILIMIA kubwa ya wafanyabiashara wa vifaa vya michezo jijini hapa wameeleza kipindi kigumu wanachopitia sasa kutokana na biashara zao kukosa wateja ‘kudorora’.
Sababu kubwa za kuyumba kwa biashara zao ni mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa Corona (Covid-19) ambao hadi sasa vimesharipotiwa visa vya wagonjwa zaidi ya milioni 3 ukisababisha vifo vya zaidi ya watu 207,391 hadi jana mchana huku 884,582 wakiripotiwa kupona.
Wakizungumza na Gazeti hili baada ya kutembelea maduka mbalimbali jijini hapa, baadhi ya wauzaji hao wamesema kuwa, mbali na shughuli za michezo kusimama lakini pia kinachowaumiza ni uhaba wa upatikanaji wa bidhaa hizo kutoka njee ya nchi.
Mfanyabiashara Yusufu Gogo anayefanyia kazi zake maeneo ya Sabasaba amesema kuwa, kwa sasa sekta ya michezo inapitia wakati mgumu sana ambao pia umeleta ugumu katika biashara zao.
Alisema kuwa, hadi sasa tayari baadhi ya wenzao wameshaanza kufunga biashara zao kutokana na kukosekana kwa wateja huku wakipanga kurejea katika biashara zao mara baada ya janga la Corona kuisha kabisa.
Alisema, kwa sasa jambo kubwa ni Watanzania kuendelea kumuomba Mungu na kuendelea kuchukua tahadhari ambazo zitawakinga watu wengi zaidi kupata maambukizi mapya ili shughuli zingine za kijamii ziweze kuendelea kama ilivyokuwa kabla ya mlipuko wa ugonjwa huo hatari.
“Kiukweli ugonjwa huu umeharibu kila kitu na kutufanya tuyumbe sana kiuchumi kutokana na kukosa wanunuzi na bidhaa zinazotoka nje kuwa adimu. Kwa sasa nadhani jambo kubwa ni kuendelea kuchukua tahadhari ili kutopata maamubiki na kuongeza idadi ya wagonjwa wapya, ” alisema Gogo.
More Stories
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship
Mnzava apania kuwapeleka vijana Simba na Yanga