November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Afya yazindua kampeni upasuaji mabusha

Na Heri Shaaban,Timesmajira Online.

MKOA wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wamezindua kampeni ya upasuaji mabusha bila malipo.

Kampeni hiyo endelevu imezinduliwa juzi katika Kituo cha Afya ya Pugu Kajiungeni wilayani Ilala.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mratibu wa magonjwa yasiopewa kipaumbele Mkoa Dar es Salaam, Alex Mkama amesema lengo lao ni kuwafanyia wagonjwa 5,000 wote wanaougua ngiri maji bure.

Alex amesema utafiti uliofanywa katika Mkoa Dar es Salaam mwaka 2015, ina wagonjwa 5,000 wa ngiri maji ambapo lengo walilojiwekea kwa mwaka huu ni wananchi 1,000 wawe wamefanyiwa operesheni hiyo.

“Kampeni hii inafanyika kila mwaka chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, mwaka huu tumeweka kambi Kituo cha Afya Pugu Kajiungeni, tunaomba wananchi wote wa kutoka wilaya zote wajitokeze katika Kituo cha Afya Pugu ambapo gharama zote zinalipwa na serikali,” amesema.

Mratibu huyo amesema katika operesheni hiyo, wanashirikiana na Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Pugu Kajiungeni, Dkt. Mingole Mutuka amesema zoezi hilo ambalo limezinduliwa jana, lilianza Machi mwaka huu na linatarajia kumalizika Mei 25 mwaka huu.

Dkt. Mutuka amesema toka kampeni hiyo ianze, kumejitokeza mwitikio mzuri ambapo wanapokea watu 20 hadi 25 na mpaka sasa, watu 334 tayari wamefanyiwa operesheni hiyo.

Amesema kinga ya kuzuia kujikinga na ugonjwa huo, ipo kwa mwaka mara moja ambapo amewashauri wananchi watumie.

Naye Daktari Bingwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Moses Antamus amesema kabla kuwafanyia operesheni hiyo wanawapa elimu baada hapo, ndiyo wanawapatia matibabu.

Dkt. Antamus amesema, baada kuwafanyia operesheni wanawapa elimu ya utunzaji kidonda ndani ya mwezi mmoja mgonjwa awe anakwenda kituo cha afya kwa uangalizi wa daktari .

Amewataka wananchi kuacha mila potofu kuhusiana na ugonjwa huo, ambao unaenezwa kwa mbu si imani za kishirikina.