Na Mwandishi Wetu,Timesmajira online Mwanza
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho amesema ujenzi wa meli ya MV Mwanza ‘Hapakazi tu’, ambao hadi sasa umefikia asilimia 74 utakamilika baadaye mwakani.
Dkt. Chamuriho ameyasema hayo jana jijini Mwanza alipokuwa akikagua ujenzi wa meli hiyo ya kisasa inayojengwa na Kampuni ya Gas Ente kutoka Korea ya Kusini, ikishirikiana na Kaang Nam Corperation pamoja na Suma JKT.
Amesema ujenzi wa meli hiyo ni moja ya miradi mikubwa minne inayotekelezwa na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) na kusimamiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
“Miradi mengine inayotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na ukarabati wa meli ya New Victoria, ujenzi wa MV Butiama pamoja na Chelezo ambayo ujenzi wake umekamilika,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Chamuriho amesema wizara pia imejipanga kuendeleza miradi mingine katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa, ikiwemo mradi wa ukarabati wa meli kongwe ya MV Liyemba.
Kwa upande wake msimamizi wa mradi wa ujenzi wa MV Mwanza, Mhandisi Vitus Mapunda amesema ujenzi huo umeajiri zaidi ya watumishi 180 katika kada mbalimbali na utakapokamilika utaleta fursa nyingi za ajira nchini.
Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa MSCL, Philemon Bagambilana amesema kampuni imejipanga kuboresha na kutoa huduma bora katika usafiri wa majini kwenye Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa, Ziwa Tanganyika na kupanua huduma kwenye Bahari ya Hindi.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea