November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbarali kushirikiana na madiwani kuondoa uhaba wa madawati

Na Esther Macha,Timesmajira Online. Mbarali

UONGOZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, umesema utashirikiana na madiwani katika kuhakikisha hakuna mwanafunzi atakayekaa chini wilayani hapa kutokana na ukosefu wa madawati.

Hayo yamesemwa jana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Itamboleo, Twalibu Lubandamo wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi ambayo kikata ilifanyika Kata ya Imalilo Songwe.

Lubandamo amesema alipoingia madarakani kama Mwenyekiti wa halmashauri, kipaumbele chake kikubwa kilikuwa madawati.

“Kwa nini nasema hivi, kwa sababu nilitembelea shule kadhaa za sekondari wilayani hapa na kushuhudia wanafunzi wanakaa chini, mwanafunzi anahitaji kukaa kwenye dawati ili aweze kupata elimu, hivyo kufika mwezi wa sita mwaka huu suala la wanafunzi kukaa chini litakuwa limekwisha,” amesema.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Imalilo Songwe ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa halmashauri, Chuki Mbwanjine amewaomba wafanyakazi wanaopata changamoto katika maeneo yao ya kazi, kutoa taarifa ili kuona jinsi ya kuwasaidia, pia kwa mvivu yeyote akibainika hawatasita kumchukulia hatua stahiki kwa kushirikiana na mamlaka husika ngazi za wilaya.

Hata hivyo Mbwanjine amewaomba Wenyeviti na Watendaji wa Vijiji kuwa pamoja kwa kujitahidi kujenga makazi ya wafanyakazi, hasa walimu angalau nyumba moja kwa mwaka kwenye vijiji vyao ili walimu waweze kukaa maeneo ya kazi na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwamba asimilia kubwa ya wafanyakazi waliopo kwenye kata zao, wanakaa mbali na makazi yao ya kazi.

Naye Diwani Viti Maalumu Kata ya Mawindi, Catherine Atilio amewataka wafanyakazi kujiunga kwenye vikundi ili waweze kukopesheka.

Diwani huyo amefafanua kuwa, ili kumwondoa mfanyakazi katika ugumu wa maisha upo muhimu wa kuona namna ya kuunda vikundi baina yao kwa ajili ya kuwapa nafasi ya mikopo ya ujasiriamali mdogo.