Na Mwandishi Wetu,TimesMajira online, Kongwa
WAZIRI wa Kilimo Prof. Aldof Mkenda amepiga marufuku kwa Jeshi la Polisi kukamata wafanyabiashara ya Mahindi wakati wanapeleka bidhaa yao sokoni kwani hali hiyo inakatisha tamaa wakulima.
Prof.Mkenda ametoa Kauli wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua na kujionea Mashamba ya Kilimo cha mkataba wa zao la mtama wilayani Kongwa.
Waziri Mkenda amesema kuwa anatarajia kuzungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) kuhakikisha jeshi hilo linaachana na tabia ya kukimbizana na wafanyabiashara hao wakati wakipeleka biashara zao sokoni.
“Kuna changamoto kubwa ya masoko inayowakabili wafanyabiashara wa mahindi nchini, wafanya biashara hao wanauhuru wa kufanya biashara eneo lolote nchini kwa kuwa wanakuwa wakitafuta masoko, hivyo kuwazuia na kuwanyang’anya mazao yao wakati wakipeleka sokoni ni kuwavunja moyo na kuwakatisha tamaa,”amesema Prof.Mkenda.
Hata hivyo Prof. Mkenda amewataka askari wa Jeshi la Polisi nchini kuacha tabia hiyo ya kuwanyanyasa na kuwasumbua wakulima na wafanyabiashara wa zao hilo ambao
wanakuwa wakipambana kujikwamua na umaskini na kuchangia pato la taifa.
“Hiki kitu kwa kweli sio kizuri hawa ni watanzania ambao wanatafuta masoko ya zao hilo ni vema wakaachiwa ili kuendelea na biashara hiyo”amesema Prof. Mkenda.
Aidha Waziri Mkenda amewataka maafisa ugani kuendelea kutoa elimu kwa wakulima wa mazao mbalimbali wilayani humo ili wafanye kilimo chenye tija ambacho kitaleta matokeo chanya kwao na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Dkt. Seleman Serera, amesema wakulima wa Kongwa wanashauku kubwa ya kuendesha kilimo cha mkataba cha zao la mtama pamoja na kilimo cha mazao mengine kitaalamu ili kusonga mbele katika kilimo.
Hivyo Dk. Serera amesema ujio wa wawekezaji hao wa ndani kutawafanya wakulima wa Kongwa kufanya kilimo cha kisasa ambacho kitaleta manufaa makubwa kwa wakazi wa eneo hilo na taifa.
Awali Mwenyekiti wa kijiji cha Sagara B, kilichopo wilayani Kongwa Bw.Gilbert Mlwande amemshukuru Waziri huyo huku akisema amewasaidia wakulima na wafanyabiashara kutatua changamoto ya kukimbizana na Jeshi la Polisi Barabarani.
More Stories
Chande azindua misheni ya uangalizi uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika
CPA.Makalla :CCM kutumia 4R za Rais Samia katika uchaguzi Serikali za Mitaa
CCM kutumia 4R za Samia Uchaguzi Serikali za Mitaa