November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi akimkabidhi mmoja wa waandishi wa habari Joyce Kiria jana mkoani Dar es Salaam.

Dkt.Abbasi: Wadau fanyieni kazi uhuru wa kiuchumi wa wanahabari

Na Mwandishi Wetu,timesmajira,Online

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, ametoa rai kwa wadau wote kushirikiana kwa pamoja kutafuta suluhu za changamoto za kiuchumi zinazovigusa vyombo vya habari.

Dkt. Abbasi ameyasema hayo Dar es Salaam jana alipokuwa akifungua semina ya wadau iliyoandaliwa kati ya Wizara na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Sayansi (Unesco) kutengeneza vipaumbele vya sekta hizo vitakavyoingia katika mipango ya kitaifa na kimataifa hasa katika utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Dunia (SDGs).

“Mara chache sana tunapofanya semina na makongamano tunakumbuka kutathmini hili kwamba uhuru wa kiuchumi wa wanahabari ni muhimu sana. Mwanahabari ambaye analipwa kiduchu, hana uhakika wa mshahara, hana bima, hana pensheni kabla hajaenda kutafuta stori tayari hana uhuru. Semina hii ilete mapendekezo namna gani vyombo vya habari viimarishe mapato yao na uchumi wao uimarishwe na pia ni muhimu mkaangalia dhana ya baadhi ya vyombo kuanzishwa kwa malengo ya mtu kisha akitimiza malengo hayo miaka miwili mitatu wanatasnia walioajiriwa wanaanza kutelekezwa na kubaki hoi. Leteni mawazo makini ili sisi Serikali tunachopaswa kufanya tutakifanya na kinachopaswa kuanzia kwa wadau wa sekta wenyewe kianzishwe,” ameahidi Dkt. Abbasi.

Katika semina hiyo ambayo ni maandalizi ya Siku ya Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yatakayofanyika Arusha Mei 3 mwaka huu, Dkt. Abbasi pia ametoa tuzo kwa wanahabari na wadau wa habari wanawake waliotoa mchango muhimu ambao ni Eda Sanga, Penzi Nyamngumi na Joyce Kiria.