November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

KMC waitaka robo fainali FA

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

BENCHI la ufundi la timu ya KMC limeendelea kukinoa kikosi chake kuelekea mchezo wao wa hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho la Azam ‘Azam Sports Federation Cup’ utakaochezwa Mei Mosi kwenye uwanja wa Jamhuri dhidi ya wenyeji Dodoma Jiji FC.

KMC inaendelea na maandalizi hayo huku mkakati wao mkubwa ikiwa ni kupata ushindi utakaowawezesha kutinga hatua ya robo fainali ambayo pia itawaongezea morali ya kufika mbali zaidi kutokana kutaka sana kuiwakilisha nchi kimataifa.

Mchezo huo utakuwa wa pili kwa timu hizo kukutana msimu huu baada ya ule wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) wa Desemba 4 ambapo Dodoma walikubali kichapo cha goli 1-0 na kisha watasubiri ule wa marudiano utakaochezwa Juni 17.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Christina Mwagala amesema, kutokana na umuhimu wa mchezo huo, Kocha John Simkoko pamoja na msaidizi wake Habib Kondo wanaendelea kuwapa wachezaji wao mbinu bora ambazo zitawasaidia kupata ushindi na kutinga robo fainali.

Ikiwa watafanikisha hilo basi watakuwa wamejisogeza zaidi karibu na hatua zinazofuata kwani mkakati wao ni kucheza fainali ili kuweza kuiwakilisha nchi katika michuano ya Shirikisho Afrika.

“Kama mnakumbuka katika mchezo wetu wa kwanza tuliwafunga goli 5-2 timu ya Kurugenzi lakini pia tumekuwa imara katika mechi zetu za Ligi Kuu hivyo tunachokitaka ni kwenda kuendeleza ushindi na morali kwani tunafahamu utakapopoteza ndio utakuwa umejiondoa kwenye michuano,”.

“Pia tunatambua kuwa hatua  hii ni ngumu zaidi ya ile tuliyotoka kwani ukiangalia timu nyingi zinazoshiriki zipo VPL na kila mmoja anamfahamu mwenzake na ndio maana tumeamua kujizatiti ili kufanya vizuri na kutwaa ubingwa wa  michuano hiyo,” amesema Christina.

Mbali na michuano hiyo, Christina amesema kuwa, pia maandalizi hayo yakuwa kwa ajili ya mechi zao zijazo za Ligi Kuu kwani hawajawa na matokeo mazuri sana katika mechi zao za ugenini za mzunguko wa pili baada ya kufungwa na kutoka sare na Mbeya City, Coastal Union na Yanga huku wakipoteza dhidi ya Tanzania Prisons na Polisi Tanzania.

Jambo hilo linafanya maandalizi hayo kuwa ya tofauti kwani wanachokitaka hivi sasa ni kupata matokeo mazuri katika mechi zao zote zilizobaki za ugenini pamoja na zile za nyumbani ambazo hawana wasiwasi nazo sana.

“Tumekuwa na kiwango bora sana katika mechi zetu za nyumbani na wachezaji wameonesha kiwango bora hivyo mipango ya benchi la ufundi ni kuhakikisha ubora huu unaendelea ugenini hivyo niwahakikishie kuwa tutapambana kupata alama tatu katika kila mchezo ulio mbele yetu,” amesema Christina.