Na Mwandishi Wetu,TimesMajira online
WATANZANIA wana kila sababu ya kujivunia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwani umewafanya watu wa Tanzania na visiwani kuwa kitu kimoja. Ni ukweli usiofichika kwamba watu wengi wa visiwa vya Pemba na Unguja asili yao ni mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Jamhuri ambayo imefanikiwa kuulinda, kuulea,na kudumisha Muungano kwa miongo mitano na nusu sasa ambapo unarithishwa kwa vizazi kwa kuwa waasisi wengi wa Muungano wametangulia mbele ya haki na kuufanya kuwa mfano wa pekee katika sayari ya dunia.
Unapoitaja Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huna budi kuwashukuru kwa dhati kabisa Waasisi wa Muungano ambao ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Shekhe Abeid Amani Karume,wanawaombea wapumzike kwa amani na hakika wataendelea kuenziwa na kuombewa siku zote za maisha yao.
Kuna faida nyingi kwa kuwepo Muungano hapa Tanzania ikilinganishwa na changamoto za hapa na pale ambazo zinatatuliwa kadri siku zinavyosonga mbele na zipo sababu nyingi zinazowafanya Watanzania kuwa wamoja, kushikamana na kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar:
Hivyo kila mwaka ifikapo Aprili 26,tunakumbuka siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambazo ziliungana Aprili 26, 1964, ambapo mwaka huu Muungano huu unatimiza miaka 57, huku ukiwa ni Muungano wa mfano na imara katika Bara la Afrika na ulimwenguni pote.
UNDUGU WA DAMU
Ipo tofauti kubwa sana kati ya Muungano wa Tanzania na nchi nyingine walioungana ambao kiasili hawana mahusiano na udugu wa damu kama ilivyo kwa Tanzania Bara na Visiwani mfano wakazi wengi wa Mji wa Tanga wana ndugu wa damu na jamaa zao walioko Unguja au Pemba, hivyo kwao mipaka na Jiografia sio sababu ya kuwatenganisha.
Wamekuwa na ushirikiano tangu hapo awali Muungano kwao umekuja kama tu kuhalalisha udugu wao kutowekewa mipaka na utaratibu wa ushirikiano kitu ambacho kimepandikizwa na wakoloni walioweka mipaka.
Aidha kutokana na tabia za kiafrika za kuhama kutoka eneo moja kwenda lingine wananchi wenye asili ya Bara wamehamia Unguja tangu enzi hizo na kuanzisha familia na kuacha baadhi ya ndugu zao Bara.
MAHUSIANO YA BIASHARA TANGU ENZI ZA WAHENGA
Biashara za aina mbalimbali zimefanyika tangu karne ya 14 ambapo wageni mbalimbali kutoka Ureno, India, Uchina, Uarabuni na Europa walifika nchini na kuwa na mahusiano na wazazi waliotangulia na kuweka makazi maeneo mbalimbali kama kule Kilwa Kisiwani ambapo Mfalme wa Ughaibuni wa Saudia aliweka makazi na kuacha kizazi chake ambacho mpaka leo kimebakia Kilwa Kisiwani na majengo yanayovutia katika utalii wa majengo ya kale ya Kilwa Kisiwani kama vile Msikiti wa Kale, na tabia, desturi, mila na taratibu za kiarabu ambazo zimesalia.
LUGHA YA KISWAHILI
Kutokana na biashara hizo zilizofanyika ingekuwa vigumu sana kusikilizana kwa kuwa kila mmoja alikuwa na lugha yake. Lakini uundwaji wa lugha ya Kiswahili kutokana na mashirikiano na mchanganyiko wa watu kutoka mataifa mbalimbali waliweza kuelewana na kusikilizana na kujenga uhusiano ambao kimsingi sio rahisi mtu mwingine yeyote kuutenganisha.
Hii ndio asili ya Mtanzania kuwa mkarimu na mtu wa kukaribisha mgeni yeyote ajaye bila kujali ametoka wapi, yeye ni nani, ana rangi gani, kabila gani au ana wadhifa gani.
Mchango wa lugha ya Kiswahili katika kukuza biashara, kuwasiliana na kuwa na mahusiano ya kifamilia ni mkubwa ambao pia umechangia kwa kiasi kikubwa kurahisisha na kuufanya Muungano wetu kuwa na nguvu na mizizi ya asili.
Mikusanyiko na watu kutoka mataifa mbalimbali kuchangamana na Watanzania.Uwepo na ujio wa wageni mbalimbali katika ardhi ya nchi zetu zote mbili,umeweka mahusiano kuwa karibu zaidi na kuweza kuoleana na kuanzisha familia ambazo zina mizizi ya nchi wanazotoka wageni hao,lakini ukizingatia mzaliwa kwao ni Tanzania iwe Visiwani au Bara.
Kama ilikuwa rahisi kwa watu wanaotoka mataifa ya mbali kushirikiana na watu wenye asili ya Zanzibar au Tanganyika inakuwa ni rahisi zaidi kuhimili undugu na uhusiano wa watu kutoka pande hizi mbili za Muungano. Nina hakika ni vigumu sana kumtenganisha mtu wa aina hii.
MATOKEO YA MAHUSIANO
Suala zima la kuoleana limeleta kufanana kwa mila, desturi, utamaduni, na mifumo ya maisha kuendeana na kufanana katika pande zote mbili za Muungano, hii imesaidia sana watu kuona kuwa ni wamoja na kuthibitisha ni tofauti tu za kijiografia, mipaka na uwanda wa Mashariki, Magharibi, Kaskazini au Kusini.
MUUNGANO NI FARAJA KWA WATANZANIA
Muungano huu ni faraja kwa Watanzania kwa kuwa umewaweka huru ndani ya nchi yao, kila mmoja ana uamuzi wa kwenda kaskazini, Mashariki, Magharibi na Kusini ili mradi havunji sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hamkwazi mtu yeyote ambaye anapashwa kuishi ndani ya Jamhuri pendwa na ya kipekee duniani ya nchi ya Tanzania.
NCHI ZILIZOWAHI KUUNGANA NA KUSAMBATARIKA
Tuangalie nchi ambazo zilijaribu kuungana duniani wakati wa karne ya 18 na 19 wimbi la kuungana lilikuwa kubwa mno na nchi nyingi duniani ziliungana na kudumu kwa muda mrefu kama ule wa Jamhuri ya Nchi za Kishosalist za Kisovieti –USSR iliyokuwa na nchi 15 zilizoungana na kugeuzwa kuwa majimbo.
Utakumbuka katika miaka ya 1990 Rais na Katibu Mkuu wa wakati huo wa nchi ya USSR Michael Gobachiev, alikuja na sera yake ya “Uwazi na Uwajibikaji” au “Glasinosis and Perestroika” ambapo alitaka majimbo hayo 15 yawe huru kila moja likijiendesha lenyewe pasipo kutegemea mfuko mkuu wa Muungano na huu kuwa chanzo kikubwa cha majimbo yaliyounda USSR kusambaratika na kurejea katika nchi zao ndogondogo za awali.
Katika suala zima la Muungano mambo ambayo yanaweza kuusambatisha ni pamoja na mifano hai kama maafa yaliyowahi kutokea katika suala zima la ubaguzi kama vile Hitler wa Ujerumani na dhana ya chuki kwa Wayahudi, Wahispania dhidi ya Waislamu, huko Hispania na Makaburu wa Afrika ya Kusini dhidi ya wazalendo Weusi wa Afrika ya Kusini huko Sharpville na yale ya Wahutu dhidi ya Watusi.
Mafanikio mengine ya Muungano ni pamoja na Watanzania kujenga umoja na misingi endelevu ya udugu baina yao,mifumo ya uendeshaji wa Serikali kwa uwazi chini ya demokrasia na utawala bora pamoja na kuongezeka kwa uelewa kuhusu umuhimu na faida za Muungano kwa umma wa Watanzania ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea na jitihada za kuelimisha umma kuhusu Muungano kupitia vyombo vya habari, semina, warsha,maonesho ya Kitaifa, ziara na machapisho.
Kupitia Muungano huu,miradi mbalimbali ya maendeleo imebuniwa na kutekelezwa na Serikali zote mbili. Baadhi ya miradi hiyo ni Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Programu za Usimamizi wa Bahari na Pwani (MACEMP), Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo na Mifugo (ASDP) na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA).
Muungano huu ni nguzo imara katika muktadha mzima wa nyanja za maisha yetu kwa kuwa umetufanya kuwa wamoja, kushirikiana, kushikamana na ni msingi wa amani na utulivu, maendeleo na mtangamano wetu na kwamba ndio unaotuimarisha.
Ili kuhakikisha kuwa Muungano wetu hautetereki, Watanzania hatuna budi kuwaenzi waasisi wa Muungano waliotuachia urithi huu, kwa kuulinda na kuudumisha kwa vitendo kwa kuwa ni nguzo na fahari pekee na ya aina yake katika Bara la Afrika.
Abdalah Kinyapi mkazi wa Kata ya Kitangiri mjini Shinyanga anasema kila Mtanzania anapaswa kuuenzi Muungano uliopo badala ya kushauri ama kushawishi uvunjike, kwani wale wote wenye nia ya kuuvunja hawaitakii mema nchi ya Tanzania.
“Kikubwa tuwaombe viongozi wa Chama na Serikali, wakati Muungano wetu unatimiza miaka 57 sasa, wajikite kwenye kumaliza changamoto mbalimbali na wazingatie kutekeleza maazimio ya Muungano,” anaeleza Kinyapi.
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika