Na Mwandishi Wetu, TimesMajira online, Dar
NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji William Ole Nasha (Mb) amewahakikishia wawekezaji kuwa Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) imejipanga kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini kwa kuwaondolea vikwazo na changamoto zinazowakabili wawekezaji.
Naibu Waziri Mhe. Ole Nasha ameyasema hayo jana Dar es Salaam katika kikao kazi kilichohusisha Menejimenti ya Kituo cha TIC pia Wakurugezi na wawakikishi wa Wakurugenzi kutoka Taasisi za Bohari ya Dawa (MSD), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kilichokuwa na lengo la kujadili kwa pamoja namna ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuweka mpango kazi ili kurahisisha uwekezaji thabiti na wenye tija kwa manufaa ya Watanzania, kikao hicho pia kimehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Godius Kahyarara.
“Tokea Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alivyoingia madarakani, uwekezaji ni moja kati masuala ambayo ameyasisitiza sana, kwamba kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wawekezaji kuwa mazingira yetu ya uwekezaji hayako sawa, hatujaweza kuvutia wawekezaji wa kutosha na hivyo kukosa fursa za kuongeza kipato, ajira na kukuza uchumi na ndio maana tumepewa siku chache ili kuhakikisha kwamba Wizara inaundwa na inasimama kuhakikisha kwamba mazingira ya uwekezaji yanaboreshwa” amesema Naibu Waziri.
Aidha, Naibu Waziri Ole Nasha amesisitiza kuwa Wizara imejipanga kusimamia miradi yote ambayo imeanza kutekelezwa na Serikali na taasisi ili kuhakikisha inaisha kwa wakati ikiwa ni moja ya maelekezo yaliyotolewa kwa Wizara hiyo ambayo wanatakiwa kisimamiwa.
Naibu Waziri Mhe. Ole Nasha ameongeza kuwa Wizara itaendelea kukutana na taasisi mbalimbali ili kuwaunganisha na Kituo cha uwekezaji Tanzania na kujadiliana kwa pamoja ni kwa namna gani wataweza kuboresha uwekezaji kwa kuzifahamu na kuzitatua changamoto mbalimbali kama ni za kisheria au kisera ziweze kurekebishwa kupitia Taasisi hizo ambazo zinatekeleza miradi hiyo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Prof. Godius Kahyarara amesema kuwa Wizara imejipanga kutekeleza maagizo na maelekezo yote yaliyotolewa na yanayoendelea kutolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni pamoja na kuondoa changamoto na vikwazo vinavyowakabili wawekezaji katika maeneo mbalimbali kama vile upatikanaji wa vibali, muda wa kupata vibali na maswala ya ardhi na mengineyo.
Prof. Godius Kahyarara ameeleza kuwa Serikali ipo mbioni kubadilisha sheria ya uwekezaji kwahiyo hiki ni kipindi cha kupata maoni kwa wanaohusika kusimamia uwekezaji ikiwemo Taasisi za umma lakini amesisitiza kuwa kwa kuunganisha nguvu pamoja na Taasisi za umma wataweza kuratibu na kusaidia kuzikabili changamoto hizo.
More Stories
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja
Gavu aanika miradi iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita Geita
RC Makongoro: Samia aungwe mkono nishati safi ya kupikia