Na Esther Macha,Timesmajira,Online,Mbeya
KAMATI ya ushauri ya wilaya ya Mbeya (DCC) imepokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa kupeleka mapendekezo ngazi ya mkoa ya kuigawa halmashauri ya jiji la Mbeya.
Katika mapendekezo hayo yaliayoazimiwa na baraza la madiwani wa halmashauri ya jiji la Mbeya mwanzoni mwa mwezi huu yanaeleza kuwa jiji la Mbeya lenye kata 36, (sasa) litabakia na kata 23 huku kata nyingine 13 zikiwa ndani ya manispaa mpya inayopendekezwa ya Uyole.
Baada ya baraza la madiwani kupendekeza kwa kauli moja mgawanyo wa halmashauri ya jiji, ilikuwa ni lazima mapendekezo hayo yapitie kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya kwa ajili ya kuyajadili kisha kuyapeleka ngazi ya mkoa ambayo nayo itawasilisha kwa waziri mwenye dhamana kwa ajili ya utekelezaji.
Akiongoza kikao cha kijadili mapendekezo, mkuu wa wilaya ya Mbeya Paul Ntinika amesema uamuzi wa kuigawanya halmashauri ya jiji la Mbeya ni utekelezaji wa agizo alilolitoa aliyekuwa rais wa Tanzania, hayati dokta John Pombe Magufuli alipokuwa ziarani jijini hapa.
Ntinika ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ushauri ya wilaya amesema baada ya kukamilisha zoezi la kuigawa halamashauri ya jiji wataanza na mchakato wa kugawa wilaya ya Mbeya ili ziwe mbili lengo likiwa ni kusogeza huduma kwa wananchi.
“Wilaya ina halmashauri mbili, ina halmashauri ya jiji la Mbeya na Mbeya vijijini, sasa leo (jana) kazi kubwa tuliyonayo ni kuja kupokea mapendekezo ya ugawaji wa halmashauri ya jiji la Mbeya pamoja na manispaa inayopendekezwa ya Uyole, kwa hiyo tutakuwa na kikao kingine kitakachokuwa na mapendekezo ya wilaya mbili,” amesema
Hata hivyo Ntinika amesema kamati yake itayafanyia kazi maoni yote yaliyotolewa na wajumbe waliohudhuria kikao hicho wakiemo viongozi wa vyama vya siasa, dini, viongozi wa kimila na baadhi ya wataalamu.
Mkaguzi wa ndani wa jiji la Mbeya, Mashaka Semkiwa ameeleza kikao hicho kuwa taratibu zote za mchakato wa kupokea mapendekezo zimefuata licha ya kuwepo kwa baadhi ya mapungufu ikiwemo ya manispaa inayopendekezwa kutokidhi vigezo.
Semkiwa amesema kwa mujibu wa sheria halmashauri ya manispaa ni lazima iwe na watu wasiopungua laki tatu na asilimia 50 ya wakazi wake wawe kwenya ajira isiyotegemea kilimo.
“Halamshauri ya jiji la Mbeya itakuwa na kata 23, mitaa 121 na eneo lenye ukubwa kilomita za mraba 127.8 na jumla ya wakazi wanaokadiriwa kufikia 280,265 na halmashauri ya manispaa ya Uyole itakuwa na kata 13, mitaa 60, eneo la kilomita za mraba ni 131 na jumla ya wakazi 243,58,” amesema
More Stories
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa
Vikundi Ileje vyakabidhiwa mikopo ya asilimia 10, DC Mgomi avipa somo