November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi wa afya waiisifu NMB kuokoa maisha ya watu

Na Mwandishi Wetu, TimesMjira Online

BENKI ya NMB imechangia kuokoa maisha ya watu kwa kutoa misaada katika vituo vya kutolea huduma za afya kwenye maeneo mbalimbali nchini ili kuboreshwa huduma hiyo na kuwawezesha Watanzania wengi kunufaika.

Akizungumzia hilo, Afisa Uwajibikaji kwa Jamii wa NMB Aloyce Kikois amesema, mpango wa uwajibikaji katika jamii ambao kitaaluma unajulikana kama Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) wenye bajeti ya takribani TZS bilioni 1 kwa mwaka.

“Katika utekelezaji wajibu wetu kwa jamii, tumejikita zaidi katika maeneo matatu ya kipaumbele ambayo ni elimu, afya na huduma jumuishi za fedha na huwa tunatenga asilimia moja ya faida ya benki baada ya kodi kwa ajili hiyo kwani tunalenga kuhakikisha tunaongeza thamani kwenye jamii husika na kuonesha uendelevu wa malengo yetu,” amesema.

Aidha amesema, lengo kuu ni kuhakikisha vifaa tiba vipo kwa ajili ya wateja wake, wadau na jamii kwa ujumla kwa kutoa vitanda vya wodini, vitanda vya kujifungulia na vifaa vingine muhimu kwa utabibu.

Kikois amesema, NMB imeamua kuchagua afya kama moja ya sekta ambazo zitapokea msaada kutokana na kuthamini umuhimu wa mama wajawazito, watoto na watu wengine wanaohudumiwa kwenye vituo hivyo na Watanzania wote kwa ujumla.

“Tunataka wateja wetu wawe na uhakika wa afya zao mwaka mzima, tunafanya nao
biashara wakiwa na afya njema, lakini wanapougua lazima wajue sisi pia tupo kwa ajili yao na ndiyo maana tumeamua kati ya faida inayopatikana sekta ya afya nayo
ifaidike,” amesema Kikois.

Banki ya NMB imetembelea taasisi zilizonufaika katika Kanda ya Kaskazini Katika kuhakikisha kunakuwepo na soko lenye afya kwa kuchangia huduma mbalimbali pamoja na mashuka na magodoro kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya pamoja na maeneo mengine mengi nchini.

Ziara hiyo imejumuisha mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha, ambapo maofisa wa NMB walitembelea vituo vinne kikiwemo kituo cha afya kilichopo katika Chuo cha Polisi (CCP) Moshi, Kituo cha Afya Pasua wilayani Moshi, Hospitali ya Wilaya Hai mkoani Kilimanjaro na Kituo cha Afya Oltrumet kilichopo Wilaya ya Arusha mkoani Arusha.

Mwakilishi wa hospitali ya Oltrumet Wilaya ya Arusha, Dk. Consolata Sweya,
amesema idadi ya magodoro, shuka na vitanda vya kulalia wagonjwa imerudisha uhai wa hospitali.

“Kwa sasa tunazalisha kwa siku kati ya wajawazito 10 hadi 13, wodi ya wazazi ina vitanda 18 ila changamoto kubwa iliyobaki ni vitanda vya watoto njiti. Hivyo tunaiomba NMB itufikirie katika eneo la watoto njiti,” amesema Dk. Sweya.

NMB imekuwa kinara wa kuwekeza katika miradi ya kijamii kutokana na ufanisi wa shughuli zake ikiwemo kuongoza kutengeneza faida ambako uiwezesha kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili hiyo ikitumia zaidi ya shilingi bilioni 5 kati ya mwaka 2015 na 2020.