Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
TANZANIA imedhamiria kukua kiuchumi hivyo kivitendo kuamua kuweka mazingira bora yanayoshirikisha sekta mbalimbali na wataalamu kwa kuweka msukumo mkubwa katika kutekeleza shughuli na miradi mbalimbali ya kiuchumi nchini.
Ni wazi kuwa masuala ya nishati katika sekta na uchumi wa nchi yoyote ni injini ya ukuaji wa uchumi ikiwa ni pamoja na ustawi wa jamii na wananchi duniani kote. Kati ya mambo makubwa yanayo chochea ukuaji wa uchumi ni pamoja na kuwa na umeme wa uhakika wakati wote.
Ili kuwa na umeme wa uhakika nchini, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambaye ndio mwenye dhamana ya kuzalisha na kusambaza umeme nchini, linahakikisha wakati wote miundombinu iko salama lakini pia na vyanzo ni vya uhakika wakati wote. Ni wazi bila usimamizi mzuri yote hayo hayatoweza kutimia kwa urahisi.
Shirika la Umeme Tanzania limejipanga na kujigawa katika maeneo makuu manne ambayo ni Kufua, Kusafirisha, Kusambaza Umeme na Uwekezaji katika miundombinu na vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme.
Akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha Wahariri Waandamizi wa Vyombo vya Habari nchini na TANESCO, Mhandisi Stephen Manda, Meneja Mwandamizi Ufuaji Umeme kutoka Shirika la Umeme, TANESCO, anasema jumla ya umeme unaozalishwa nchini ni Megawati (Mw) 1,604.81.
“Katika gridi ya Taifa, TANESCO ina jumla ya Mw 1,393.45, na kampuni binafsi ya Independent Power Producers (IPP) ina Mw.211.36 kutokana na vyanzo mchanganyiko ambavyo ni maji, gesi asilia, mafuta mazito pamoja na tungamotaka (biomass).” Amesema Mhandisi Manda
Katika Gridi ya Taifa, TANESCO inamiliki umeme asilimia 86.5 (ambayo ni sawa na Mw 1,356.589) huku ikiwajibika kusimamia, kutunza na kuendeleza miundobimu ya umeme, na asilimia zilizobaki kumilikiwa na kampuni binafsi.
Ni mikoa mitatu tu ndio ambayo bado haijaungwa katika gridi ya taifa ambayo ni Mkoa wa Kigoma ambako umeme unapatikana kupitia mitambo ya mafuta pamoja na Mkoa wa Katavi na Rukwa.
“Kuna jitihada (miradi) mbalimbali inaendelea Ili kuhakikisha mikoa hiyo inaungwa katika Gridi ya Taifa,” anasema Mhandisi Manda na kwamba kwa kufanya hivyo mitambo inayoendeshwa kwa mafuta itazimwa hatua ambayo itaipunguzia serikali gharama kwani kuzalisha umeme wa mafuta ni gharama kubwa.
Mpaka kufikia Desemba 22,2020, mahitaji ya juu kabisa ya umeme nchini ni Megawati (Mw)1,180.53 ikimaanisha kuna ziada ya Mw 200, baada ya kuondoa kiwango cha ziada kama ikitokea dharura.
Kwa sasa chanzo kikubwa cha ufuaji umeme nchini ni Gesi ambayo inachangia asilimia 56 (Mw 901.32), ikifuatiwa na Maji kwa asilimia 36 (Mw573.71), Mafuta mazito ni asilimia 7 (Mw 119.28) pamoja na Tungamotaka kwa asilimia 1 (Mw 10.5)
Mhandisi Manda anasema, “hali hiyo ni ya muda tu kwani kufikia Juni,2022, umeme unaotokana na maji ndio utakuwa mwingi zaidi baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa Julius Nyerere ambao utazalisha umeme wa Mw 2,115 kwa kutumia maji.”
Pia vyanzo vingine vya kuzalisha umeme kama jotoardhi na upepo na hata jua, vianonesha dalili ya kuchangia umeme jambo ambalo litabadili taswira ya uchangiaji umeme katika uzalishaji.
HALI YA UFUAJI UMEME NCHINI
Hali ya ufuaji umeme nchini ni nzuri kwani inawezesha kupatikana umeme wa uhakika katika vipindi vyote.
Mpaka sasa kuna vyanzo saba vya kuzalisha umeme wa maji (Hydro plants) ambavyo kwa ujumla vinazalisha Mw 561.843, pia kuna vyanzo saba vya gesi asilia vinavyochangia Mw 712.32, vyanzo 10 vya mafuta mazito Mw 87.96. Lakini pia kuna mitambo ambayo haijaungwa katika gridi ya taifa ambavyo ni vya mafuta mazito (isolated power station) vinavyozalisha Mw. 33.13
Ili kuokoa au kupunguza hasara katika uendeshaji wa Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO) imefanikiwa kufunga na kuzima baadhi ya mitambo ya kuzalisha umeme unaotumia mafuta mazito katika Mkoa wa Ruvuma na kuungwa katika gridi ya taifa kutokea Makambako kwa msongo wa 220 Kv, Mbinga pia iliotolewa katika matumizi ya umeme wa mafuta, Madaba, Liwale, ikiwa ni pamoja na Songea.
Mhandisi Manda anasema “Mitambo iliyobaki na inaendelea kuzalisha umeme wa mafuta mazito ni Nyakato, Zuzu, Biharamuro na Ngara.”
Mitambo iliyopo nje ya gridi ya taifa iko Kasulu, Kibondo, Kigoma, Loliondo (Arusha), Mafia(Pwani) na Mpanda (Katavi). Mingine ni Sumbawanga(Rukwa), Bukoba(Kagera) na Inyonga(Katavi). Jumla ya mitambo hii inazalisha jumla ya Mw 33.13.
HALI HALISI YA MABWAWA
Tangu mwaka 2019/2021 hali ya maji katika mabwawa yanayozalisha umeme ni nzuri. Hii ni kutokana na mvua zilizonyesha katika mwaka 2019/ 2020. Hali ya maji imekuwa nzuri mpaka kufikia kufungulia maji ili yasilete madhara katika mabwawa na jamii na kusababisha hasara kubwa.
Mhandisi Manda anasema, “Mpaka kufika Februari 26, 2021 Bwawa la Mtera lilikuwa limejaa maji kiasi cha kufikia ujazo wa 698.76 mita za ujazo kutoka usawa wa bahari (masl) ambapo kiwango cha juu kabisa ni 698.5masl hivyo mpaka sasa maji yamepitiliza kiwango halisi na kulazimika kufungulia/kupunguza maji ili kulilinda bwawa pamoja na miundombinu”.
“Bwawa la Kidatu 448.81 mita za ujazo kutka usawa wa bahari (masl) ambapo uwezo wa juu kabisa ni 450masl hivyo na penyewe panalazimika kupunguzwa maji. Mengine ni Nyumba ya Mungu 685.62masl ambapo uwezo wa bwawa kuhifadhi maji ni 688.91masl na New Pangani Falss 177.40masl ambapo uwezo wa bwawa ni 177.50, ambapo kuna tofauti ya sentimita 10.
“Hivyo kwa ujumla hali ni nzuri katika mabwawa yetu. La muhimu ni kuhakikisha umeme unapatikana kwa uhakika kabisa ili kukidhi mahitaji ya taifa kwani uwezo upo” anasema Mhandisi Manda.
Ili kuhakikisha mitambo inazalisha umeme wa uhakika bila usumbufu, ni muhimu kuhakikisha inahudumuwa kwa wakati. Shirika la Umeme Tanzania limepanga kufanya marekebisho katika mitambo pamoja na miundombinu mbalimbali katika kipindi cha mwaka 2020/2021.
Katika kukabiliana na changamoto za uendeshaji wa Shirika la Umeme na kupunguza gharama za uendeshaji na uzalishaji, TANESCO imejipanga kwa kuzigeuza changamoto ilizonazo kuwa fursa.
Kati ya mambo yanayoongeza gharama na kupunguza faida ya shirika hilo ni pamoja na kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme ambayo haipo katika gridi. Mitambo hiyo kwa muda mrefu imekuwa ikiendeshwa kwa kutumia mafuta mazito ili kufikisha umeme katika maeneo ambayo hayapo katika gridi ya taifa.
Hivyo shirika linaendelea kutanua wigo na mtandao wake katika miradi inayoendelea katika njia ya umeme wa msongo wa Kv 132 kutoka Tabora kuelekea Katavi pamoja na Mkoa wa Kigoma. Kwa kufanya hivyo TANESCO itaweza kutekeleza azma yake ya kuzima au kuacha kutumia umeme wa mafuta mazito katika mikoa ya Rukwa, Katavi pamoja na Kigoma.
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika