November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nishati ya jotoardhi, fursa mpya kwa uchumi nchini

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

NISHATI ya umeme ni moja ya nyenzo muhimu katika maendeleo ya uchumi katika taifa lolote duniani.

Hata hivyo hapa Tanzania kwa kipindi kirefu huko nyuma nchi yetu ilikuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa nishati hiyo na kusababisha vipindi vingine nchi kuingia katika umeme wa mgao.

Uhaba wa umeme uliokuwa ukilikabili taifa ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na kutokuwa na vyanzo vya kutosha vya kuzalisha nishati hiyo mbali ya vichache vilivyokuwepo mfano Bwawa la Kidatu kule mkoani Morogoro.

Kutokana na uhaba huo viwanda vingi vilivyokuwepo wakati vilikuwa vikizalisha chini ya kiwango na hivyo uzalishaji wake kutokuweza kuleta faida kubwa ambayo pia kwa upande mmoja ingechangia katika pato la taifa kutokana kodi na tozo nyingine ambazo Serikali ingelipwa.

Waziri wa Nishati Dk. Medard Kalemani akigusa maji ya moto katika mojawapo wa chemchem ya majimoto ambacho ni chanzo cha nishati ya jotoardhi katika enelo la Majimoto mkoani Songwe, katikati ni Meneja Mkuu TGDC Mhandisi Kato Kabaka na Kaimu Mkurugenzi Maendeleo ya Biashara TGDC Mhandisi Shakiru Kajugus (kushoto). Picha ya Maktaba

Ili kuondokana na adha hiyo serikali kupitia Wizara ya Nishati ilifanya chini juu kuongeza vyanzo vitakavyotumika kuzalisha umeme ili kupatikana umeme wa kutosha na kuwezesha wananchi kuondokana na adha ya umeme wa mgao huku viwanda vikizalisha chini ya uwezo wake.

Baadhi ya vyanzo vilivyokuwa vikipewa kipaumbele ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa maji pamoja na uzalishaji umeme kwa kutumia makaa ya mawe, gesi asilia, urani, nishati ya jua, upepo na nishati ya jotoardhi.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Shirika la Umeme nchini (TANESCO) uzalishaji umeme kwa kutumia maji una uwezo wa kuzalisha 4.7GW, mlimbiko wa makaa ya mawe unakadiriwa kuwa tani milioni 1,200, ambapo tani milioni 304 zimethibitishwa huku gezi asilia ikikadiriwa kuwa mita za ujazo bilioni 45. 

Katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na umeme wa kutosha, baada ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli kuingia madarakani ilikuja na mkakati kabambe wa kujenga chanzo cha uhakika cha umeme katika mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) ambao kwa sasa unafahamika kama Mradi wa kuzalisha Umeme wa Maji wa Julius Nyerere(JNHPP).

Mradi huu pamoja na miradi mingine inayoendelea kutekelezwa hapa nchini ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo imelenga kufanikisha utekelezaji wa sera ya viwanda hususani kupitia miradi ya nishati ya umeme na unategemewa kuwa njia sahihi ya kufikia uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Baadhi ya watalii wakifurahia chemchem ya majimoto ya Rundugai au Kikuletwa (chemka) Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro. Picha kwa hisani ya Mtandao

Katika moja ya taarifa zake za hivi karibuni Waziri wa Nishati nchini, Dkt. Medard Kalemani alinukuliwa akieleza kuwa Serikali imekusudia kuhakikisha Tanzania inazalisha megawati 5,000 za umeme ifikapo mwaka 2025 ambapo nchi wakati huo itaweza kuuza umeme wake katika nchi jirani.

Hata hivyo pamoja na matarajio hayo, bado mikakati mbalimbali imekuwa ikifanyika kwa lengo la kuiwezesha nchi kuwa na vyanzo vingi ya nishati ya umeme sambamba na matumizi ya nishati mbadala inayopatikana hapa nchini.

Moja ya mikakati hiyo ni pamoja na kuanza utengenezaji wa nishati inayotokana na Jotoardhi, ambayo kwa sehemu kubwa nishati hii haifahamiki na wananchi wengi lakini kiuhalisia tayari baadhi ya maeneo imeanza kutumika na kuonesha matokeo mazuri.

Matumizi ya nishati ya jotoardhi ni moja ya juhudi za serikali kutaka kuliwezesha taifa la Tanzania kujitosheleza kwa nishati ya umeme hali ambayo itawezesha watanzania kuipata nishati hiyo kwa bei nafuu na hivyo kuongeza kasi ya ukuwaji wa uchumi wa Taifa.

Akiwasilisha mada katika moja ya kongamano lililowahusisha Wahariri wa vyombo vya habari nchini, Meneja Mkuu wa Kampuni tanzu ya Shirika la Umeme ambayo ni kampuni inayoshughulika na nishati ya Jotoardhi (TGDC), Mhandisi Kato Kabaka, anasema mfumo wa jotoardhi ni mfano wa kuendesha injini yoyote kwa kutumia mvuke ‘steam engine’.

Nishati ya joto ardhi ni joto linatokana na joto la asili ambalo liko kwenye dunia.Dunia yetu ina joto jingi linalofika nyuzi joto 6000.

Ziwa Ngozi liko Mkoa wa Mbeya ni moja ya vivutio vikubwa nchini kwani katika ziwa hili kuna jotoardhi na linatoa maji moto kwa chini ingawa juu maji ni baridi lakini chini ni moto. Picha ya Mtandao

Mhandisi Kabaka anasema matumizi ya nishati ya Jotoardhi yana faida kuu za msingi tatu ikiwemo kusaidia kuchangia uchumi wa nchi, ustawi wa jamii na kupatikana kwa nishati jadidifu, hivyo kutunza mazingira.

“Matumizi ya Jotoardhi ni mengi na hutegemea kiasi cha joto kinachopatikana. Kuanzia nyuzi joto 20 unaweza kuchemsha maji kwa matumizi ya nyumbani kama vile kudhibiti baridi ambapo mtu hutakiwa kuweka bomba maalumu tu linaloingia ndani na baadaye maji yanayotoka yanarejeshwa ardhini.

“Kwa watu wanaoishi maeneo yenye baridi kali mfano Mikoa ya Kanda ya Kusini na kwingine ukitumia mfumo wa jotoardhi huhitaji kupata nyuzi joto 100 kupata joto, kwa mfumo huu digrii 40 zinatosha kukupatia joto la kutosha” anaongeza

“Lakini pia Jotoardhi kati ya digrii 30 hadi 60 linaweza kutumika katika bwawa maalumu la kuogelea ambapo maji yake huja na madini mengi na huwa mazito hivyo mtu anapokuwa ndani huweza kumuinua juu na kumpa burudani,’ anasema

Joto hilo pia linaweza kutumika kukausha mazao ukitumia nyuzi 80 wakati kwa umeme joto linalohitajika ni nyuzi joto 100. Mfano ni nchi ya Iceland ambapo wanatumia mfumo huu kuzalisha umeme na baada ya hapo wanakausha samaki na kisha kusafirishwa kuwauza nchini Nigeria.

Zipo nchi 11 katika bonde la Ufa la Afrika, ambapo kwa Afrika Mashariki Tanzania ni mojawapo, ambazo tayari zimeanza kutumia mfumo wa Nishati ya Jotoardhi kuzalisha umeme na matumizi mengine ya kiuchumi na kijamii ikiwemo kutoa suluhisho la hali ya hewa.

Mhandisi Kabaka anasema lengo la kampuni yake ni kuzalisha megawati 200 ifikapo mwaka 2025 ambapo pia wataweza kuangalia matumizi mengine yenye manufaa kwa jamii na uchumi wa nchi yatakayowezesha kufunguliwa kwa fursa nyingine kwa wananchi wa Tanzania.

Mpaka sasa duniani kuna nchi 90 zenye uwezekano wa kupata jotoardhi lakini ni nchi 26 tu zimeanza uzalishaji zikizalisha megawati 14.6 kwa ajili ya umeme ambapo kwa Afrika ni Kenya ndiyo inaongoza kwa kuzalisha Megawati 800.

Pamoja na kwamba Kenya inaongoza, si jambo la kushangazi kwani wao hawana vyanzo vingi kama nchini kwetu, Kenya ilichoronga shimo la kwanza kwa ajili ya nishati ya jotoardhi mwaka 1956 na kuzalisha umeme wake mwaka 1981,  hii ilikuwa ni safari ndefu sana.

Kabaka anasema, hata hivyo kwa vile hawakuwa na vyanzo vya gesi ilibidi Kenya iweke nguvu zao na kuwa moja ya sababu ya kutangulia na kwa sasa Tanzania imeanza mchakato wa kupata jotoardhi na yapo mambo ya msingi yanayohitajika ambayo tayari serikali imeyatekeleza.

“Jotoardhi ni nishati endelevu na ya uhakika kwa vile dunia haiwezi kupoa joto lake, muda wote joto lipo, hivyo umeme wa jotoardhi utaendelea kuwepo masaa ishirini, siku saba, mwaka mzima dunia haiwezi kupoa na haitapoa,

“Na tuelewe kuwa nishati hii inafaa kwa ajili ya matumizi ya gridi na ni rafiki wa mazingira kwa vile gesi ya hewa ya ukaa inayotoka kwenye jotoardhi ni kiasi kidogo sana ikilinganishwa na vyanzo vingine,Mhandisi Kabaka anaeleza.

Anasema umeme wa jotoardhi itabidi uanzie kuzalishwa pale unapofikia digrii 100 na unaweza kwenda na kuunganisha umeme hadi kufikia digrii 350 ukizidi hapo unakuwa na shida kidogo japokuwa kabla ya hapo kuna matumizi mengine ambayo unaweza kutumiwa.

Anafafanua kuwa mpaka sasa kwa hapa nchini wameanza kutumia nishati hiyo kwa matumizi mengine na wamefikia kiasi cha digrii 80 na wanaendelea kuelekea kwenye umeme na kwamba kwa kawaida matumizi ya jotoardhi hutegemea uko wapi na unataka kufanya nini na uchumi wa pale ni wa kitu gani kinachoendelea.

Nishati ya umeme wa jotoardhi inaweza kutumika katika matumizi mengine mfano kukaushia mazao, kilimo, ufugaji viwandani na utalii na inategemea nyuzi za joto utakazokuwa nazo kwenye sehemu husika na mara zote hausababishi uchafuzi wa aina yoyote wa mazingira.

Kwa sasa mradi huo upo katika hatua ya pili umekamilika na baada ya hapo itafuata hatua ya uzalishaji.

Kabaka anasema kuwa Serikali iliona ni vyema kuwa taasisi hiyo ikawa chini ya TANESCO kwa sababu inataka kuzalisha umeme na basi nguvu na msukumo utakuwepo na matokeo yatapatikana.

mwisho